Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Balozi Seif Idd Ataka Wazalishaji Viungo Kujitangaza Kimataifa
Jul 10, 2017
Na Msemaji Mkuu

Frank Mvungi-Maelezo

Wazalishaji wa Viungo wametakiwa kutumia uwepo wa fursa ya soko la Kimataifa Kutangaza na Kuuza bidhaa zao ili kuchangia katika kukuza achumi na ajira nchini.

Akizungumza wakati akifungua maadhimisho ya siku ya Viungo katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ally Iddi, amesema soko la bidhaa za viungo nje ya Tanzania ni kubwa na linaweza kusaidia katika kufanya bidhaa hizo kukuza uchumi na kuzalisha ajira zaidi.

“Masoko nje yapo na katika hili nasikitika kwamba kuna watu wameingia kwenye biashara hii na wanakuwa madalali wakuchukua bidhaa za viungo na kwenda kuuza nje na kuwaacha wazalishaji mkiwa hamnufaiki kwa kiwango cha kutosha, sasa ni muhimu tuwaondoe watu hao ili wazalishaji mnufaike,” alisisitiza Balozi Iddi.

Akifafanua Zaidi Mhe. Balozi Iddi alisema kuwa kwa sasa kuna umuhimu wa kuweka mkazo katika kuzalisha mazao ya viungo kwa kuwa soko lipo na linaendelea kukua hali itakayosaidia kuwainua wananchi wanaoshiriki katika kuzalisha viungo.

Aliongeza kuwa kilichovutia zaidi ni kuwepo kwa siku hii maalum ya viungo inayohamasisha Watanzania kutumia viungo vya Tanzania ili kuwaongezea ari wazalishaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya usindikaji hapa nchini.

Akifafanua Balozi Iddi amesema kuwa kuwepo kwa nchi 30 katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam ni ishara kuwa sasa maonesho hayo yanazidi kukua mwaka hadi mwaka kutokana na maandalizi mazuri yanayofanywa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE).

Maadhimisho ya siku ya Viungo yanaadhimishwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya maonesho ya Kimataifa ya 41 ya Dar es Salaam yanayofanyika katika viwanja vya JK Nyerere, Barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi