Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Mhandisi John Kijazi leo tarehe 28/08/2018 amemtembelea na kumjulia hali Dkt Hamisi Kigwangalla ambaye anapata matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI akiuguza majeraha ya mkono aliyopata katika ajali iliyotokea Agosti 4, mwaka huu Mkoani Manyara.
Balozi Kijazi amempa pole Mh Dkt. Kigwangalla na kumtakia heri na apone haraka ili aweze kurejea kwenye majukumu yake ya kila siku kwani Taifa linauhitaji mchango wake.
“Pole sana. Mungu atajalia utapona na utarejea nyumbani mapema, na kwa kuwa wewe ni daktari ukiona hali si nzuri utawafahamisha wenzio mapema ili mjadiliane namna ya kuikabili hali itakayojitokeza” Alisema Balozi Kijazi wakati wa kumjulia pole Hospitalini hapo.
[caption id="attachment_34549" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu Kiongozi nchini, Balozi Mhandisi John Kijazi akishuhudia picha ya X ray inayoonesha eneo la mkono wa kushoto wa Waziri Dkt. Hamisi Kigwangalla anayepatiwa tiba MOI namna unavyoendelea. Aliyeshika Xray ni Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface, wengine ni Mkurugenzi mtendaji wa Muhimbili, Profesa Laurence Museru na Mkurugenzi wa Tiba MOI Dkt. Samuel Swai. Mapema leo Agosti 28,2018, Wakati alipomtembelea Wodi ya Kitengo cha Mifupa MOI.[/caption]Aidha, Balozi Kijazi amemueleza Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Respicious Boniface kwamba kwa sasa wananchi wanaridhishwa na huduma zinazotolewa na MOI na Muhimbili kwa ujumla na hii ni faraja kubwa kwa Serikali na hivyo kuelekeza ari hiyo iendelezwe.
“Pamoja na Jitihada kubwa za Mh Rais Dkt John Pombe Magufuli za kuboresha huduma za Afya hapa nchini, nanyi pia kwa upande wenu mnajitahidi sana na wananchi wanaridhishwa na huduma mnazotoa. Nafahamu kuna changamoto chache lakini bado mmeendelea kufanya kazi nzuri” Alisema Balozi Kijazi.
Kwa upande wake, Dkt Hamis Kigwangalla amemshukuru Balozi Kijazi kwa kumtembelea na kumjulia hali na amemueleza kwamba afya yake imeendelea kuimarika na anaamini katika kipindi kifupi kijacho madaktari watakapojiridhisha wanaweza kumpa ruhusa ya kutoka hospitalini.
“Ninaendelea vizuri, afya yangu inaimarika siku hadi siku, na pia naendelea na mazoezi na kila siku najiona imara zaidi na hii ni ishara tosha kwamba ninaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani” Alisema Dkt. Kigwangalla.
[caption id="attachment_34548" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu Kiongozi nchini, Balozi Mhandisi John Kijazi akitoa maelekezo kwa jopo la Madaktari Bingwa na Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na Taasisi ya Mifupa ya MOI ambao wanamtibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (Aliyeketi) alipomtembelea mapema leo Agosti 28,2018, Wodi ya Kitengo cha Mifupa MOI.[/caption]Dkt. Kigwangalla alihamishiwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI tarehe 12/08/2018 baada ya kupata matibabu ya awali katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kwa sasa bado anaendelea na tiba kuuguza mkono wake wa kushoto.