Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

BAKITA Watakiwa Kushirikisha Wadau Kuboresha Mkakati wa Ubidhaishaji Kiswahili
Aug 23, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa ameliagiza Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuwashirikisha wadau wa lugha ya Kiswahili katika kuboresha Mkakati wa Taifa wa Miaka 10 wa ubidhaishaji Kiswahili ili baada ya hapo uzinduliwe na kuanza kutekelezwa.

Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo katika kikao na watendaji wa Baraza hilo kilichofanyika ofisi za BAKITA Jijini Dar es Salam ambapo aliambatana na Naibu wake Mhe.  Pauline Gekul.

Pamoja na kuagiza ushirikishwa wa wadau katika uboreshaji wa Mkakati huo, Waziri Bashungwa pia amewaagiza BAKITA kufanya maboresho kadhaa, ikiwa ni pamoja na kuongeza ufunguzi wa vituo maalum vya kufundishia lugha ya Kiswahili na Utamaduni wa Mtanzania katika nchi mbalimbali Duniani.

Mkakati huo unaopendekezwa na BAKITA unalenga kubidhaisha lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 2021-2031 ambapo lugha hiyo kwa miaka ya hivi karibuni imeanza kutumika maeneo mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Bi. Consolata Mushi, baada ya kupokea maelekezo ya viongozi hao, hatua inayofuata ni kuwapitisha wadau wa Kiswahili katika mkakati huo kabla ya kuuwakilisha kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi kwa ajili ya hatua zaidi za kiutendaji na utekelezaji wa mkakati huo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi