Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Aweso Aagiza Mradi wa Maji Kyaka Bunazi Kukamilika kwa Wakati
Jan 27, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na Allawi Kaboyo – Missenyi.

Waziri wa maji, Jumaa Aweso amemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji Kyaka Bunazi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa muda ambao umepangwa kwa mujibu wa mkataba na kusisitiza kuwa hakutokuwa na muda wa nyongeza kwenye mradi huo.

Mhe. Aweso ametoa maagizo hayo Januari 26, mwaka huu alipotembelea mradi huo ili kujionea maendeleo yake akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Nadhifa Kemikimba, ambapo mradi huo unajengwa na Mkandarasi aitwaye China Civil Engineering Consultant & Cooperation na kusimamiwa na Mamlaka ya Maji Mwanza kwa gharama ya shilingi bilioni 15.1 hadi kukamilika kwake.

Aweso amesema kuwa mradi huo unatakiwa kuisha haraka na kuanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi husika hivyo wao kama wizara hawatakuwa kikwazo cha wananchi kukosa huduma hiyo ya maji kwa kisingizio chochote.

“Ikumbukwe kuwa mradi huu ni ahadi ya Mhe. Rais Magufuli na tayari mradi upo kwenye ilani, na siku chache zilizopita Mhe. Rais alipita hapa akauliza maendeleo ya mradi huu, kimsingi hakuridhishwa na kasi yake na akatoa maelekezo, kwanza niseme tu maelekezo hayo tumeyapokea na tunayatekeleza na ndio maana mimi Waziri mwenye dhamana ya maji niko hapa, nikuombe Mkandarasi tusije tukaonana wabaya nataka mradi huu ukamilike kwa wakati uliopangwa ikiwemo pia kupitia upya gharama za mradi”, amesema Waziri Aweso.

Akitoa taarifa ya mradi kwa Waziri, Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA, Leonard Msenyele ambaye ni Msimamizi Mkuu wa mradi huo amesema kuwa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 35% ambapo Mkandarasi anatakiwa kujenga chanzo cha maji katika kingo za  mto Kagera, kulaza bomba la kilomita 1.6, kujenga mtambo wa kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha  lita milioni 6.57 kwa siku na tanki la kuhifadhia maji safi lenye ujazo wa lita milioni 2.

Msenyele ameongeza kuwa Mkandarasi atatekeleza kazi hizo kwa gharama ya shilingi bilioni 9.4 huku akisisitiza kuwa malengo yao ni kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya miezi 6 iliyobaki na anauhakika watamaliza.

Akiongea na watumishi wa walioko chini ya wizara hiyo katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Waziri Aweso amewataka watumishi hao kuwa waaminifu na wabunifu katika kutekeleza miradi ya maji kwenye maeneo yao ili kuhakikisha wananchi wananufaika na pesa inayotolewa na Serikali yao.

Amewataka Mameneja wa wilaya zote za mkoa huo kufikia Machi 22 mwaka huu ambayo itakuwa ni siku ya kilele cha wiki ya maji, kuhakikisha wawe wamekamilisha miradi yote ya maji inayoendelea hasa miradi  kichefuchefu na kuitumia siku hiyo kuikabidhi na kuzindua miradi  hiyo ikiwa inatoa maji safi na salama na yenye kutosheleza.

Aidha, amewaagiza Mameneja wa Mamlaka za Maji wa Mikoa na Wilaya pamoja na Mameneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) wa mikoa na wilaya kujenga tabia ya kuongea na watumishi wao kuhusu mwenendo mzima wa utekelezaji wa majukumu yao huku akiwataka pia kuboresha maslahi  yao sambamba na kuwapa motisha pale wanapofanya vizuri.

Awali, Waziri Awezo alipokea taarifa mbalimbali za maji kutoka RUWASA, MAABARA, BONDE na BUWASA ambapo wameeleza mafanikio makubwa waliyoyapata katika kipindi hiki cha miaka mitano huku BUWASA wakibainisha changamoto kubwa inayowasumbua ya ulimbikizaji wa madeni hasa taasisi za serikali moja wapo ikiwa ni Magereza Bukoba ambayo inadaiwa zaidi ya shilingi milioni 9.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi