Anwani za Makazi kuwa Msingi wa Utambuzi wa Kila Mwananchi
Na Prisca Ulomi, WHMTH, Morogoro
Serikali imejikita kutekeleza mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi nchi nzima kwa lengo la kuibadilisha Tanzania kuwa ya kidijitali kwa kuwa anwani za makazi na postikodi ni msingi wa utambuzi wa kila mwananchi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ambaye amewakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kwa viongozi, watendaji na wataalam wa Mkoa wa Morogoro kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi.
Dkt. Yonazi amesema kuwa anwani za makazi na postikodi ni msingi wa utambuzi ili kila mwananchi aweze kutambuliwa pale alipo ambapo nia ya Serikali ni kuihakikisha kuwa kila mtaa, barabara, inakuwa na jina la mtaa na kila nyumba inakuwa na namba ya nyumba.
Vile vile, ameitaka Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro kusimamia utekelezaji wa mfumo huu ili ifikapo mwezi Mei mwaka huu jambo hili liwe limekamilika kwa kuwa utekelezaji wa mfumo huu utaiwezesha Serikali kuwa na sensa bora ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
.
Ameongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inayoratibu jambo hili, imeelekeza taasisi zote za Serikali nchi nzima zinatekeleza mfumo huu wamiliki wote wa majengo na nyumba nao waweke namba za nyumba kwenye nyumba na majengo yao na wataalam wote waliojengewa uwezo watumike vizuri kutekeleza mfumo wa anwani za makazi na postikodi na jambo hili liwe ajenda kwenye vikao.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bi. Mariam Mtunguja akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela amesema kuwa kimsingi tumechelewa kutekeleza mfumo huu wa anwani za makazi, ila kwa kuwa viongozi mtajengewa uelewa, ni matumaini yangu kuwa kwa pamoja tutashirikiana na wataalam wetu kutekeleza jambo hili kwenye maeneo yetu ndani ya muda uliopangwa na niahidi kuwa Mkoa wa Morogoro hatutawaangusha Wizara.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi, amesema kuwa mfumo wa anwani za makazi na postikodi ni moja ya aina ya mawasiliano kama zilivyo aina nyingine za mawasiliano na mfumo huu unahusisha eneo husika ambapo utamuwezesha mwananchi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine; utarahisisha shughuli za kiuchumi, kijamii na utawala
Wakitoa salamu za shukrani kwa niaba ya viongozi wengine, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini Fikiri Juma, amesema kuwa viongozi watoe majina ya mitaa ndani ya siku moja ili kufanikisha utekelezaji na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga amesema watahamasisha wananchi kununua vibao vya nyumba ili kufaniisha uwekaji wa mfumo wa anwani za makazi kwenye Mkoa huo