Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha mfumo wa utoaji haki hapa nchini unaimarika na kuwatendea haki wananchi wote.
Mhe. Rais Samia ameeleza azma hiyo leo Julai 15, 2023 Ikulu, Dar es Salaam baada ya kupokea mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Haki Jinai.
"Niliipa Tume kazi ya kuangalia mwenendo wa utekelezaji wa masuala ya Haki Jinai nchini na kuangalia jinsi haki inavyotolewa”, ameeleza Rais Samia.
Ameeleza kuwa mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo yamegawanyika katika maeneo makuu mawili ambayo yanataka mageuzi makubwa ambayo ni eneo la kiutawala na kiufundi na kusisitiza kuwa lazima mageuzi hayo yaanze na sisi wenyewe (watendaji wa Serikali) ili kuondoa udhaifu tulionao katika utendaji kazi, ili haki iweze kutendeka.
Kuhusu matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi, Mhe. Rais ametaka suala hilo liangaliwe upya kwani wapo wanaopitiliza, wajitathmini na elimu itolewe na kutungwa kwa sheria
Aidha, Mhe. Rais Samia ametaka Jeshi la Polisi kufanyiwa thathmini na kurekebishwa ili lisimame vizuri na kuboresha masuala yao ikiwemo mafunzo, utendaji, mishahara na stahiki zao ili Jeshi lifanye kazi zao vizuri.
Sanjari na hilo, amesema Serikali itaunda kikundi maalum cha kushughulikia masuala kuhusu makubaliano ya kukiri makosa ili kuona jinsi ya kuweka mambo sawa katika upatikanaji wa haki.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Samia amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi kukaa na Kamati iliyowasilisha ripoti hiyo na kuunda Kamati ndogo zitakazoangalia mapendekezo yaliyotolewa ili kujua ya kufanyiwa kazi na Serikali moja kwa moja na yale ya kubaki mikononi mwa Kamati kwa ajili ya utekelezaji.
Amevitaka Vyombo vya Habari ikiwemo TBC, Channel Ten na vingine kuwatumia Wajumbe wa Tume ya Haki Jinai kuchambua masuala yote yaliyowasilishwa ikiwemo mapendekezo yake ili Watanzania wasikie na kujua mwelekeo wa Serikali katika kuwatumikia Watanzania.