Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Arusha Inahitaji Uwekezaji Mkubwa Kuimarisha Utalii
Nov 01, 2023
Arusha Inahitaji Uwekezaji Mkubwa Kuimarisha Utalii
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella akizungumza leo jijini humo.
Na Elinipa Lupembe - ARUSHA

Mkuu wa  Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella, amesema kuwa mkoa huo kwa sasa unahitaji mpango mkakati wa uwekezaji mkubwa  kisekta, hususani katika miundombinu ya barabara, makazi na rasilimali watu ili kuboresha sekta ya utalii na kumudu kuwahudumia wageni.

Mhe. Mongella amesema hayo leo jijini Arusha na kuwataka wadau na wakazi wa Arusha, kuungana kuwa na mpango endelevu wa kuwekeza kwenye katika sekta zote zinazoweza kulisha sekta ya utalii.

Ameweka wazi kuwa, serikali imetoa fedha za  mradi mikubwa ya kimkakati  wa Jiji la Arusha ili kuboresha miundombinu na kuwataka wadau na wakazi wa mkoa huo kutumia fursa kuwekeza kwenye sekta zote zinazolisha sekta ya Utalii.

Amefafanua kuwa, Utalii ndio muhimili wa uchumi wa mkoa huo na Tanzania kwa ujumla, hivyo kunahitajika, uwepo wa miundombinu ya uhakika, kwa kujenga hoteli za kutosha zenye hadhi, barabara za kupitika kipindi chote pamoja na kuwa na rasilimali watu ya kuwahudumia wageni hao.

Ameongeza  kuwa kwa sasa mkoa umefunguka kiuchumi, unapokea wageni wengi kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo kuna uhitaji wa kufanya uwekezaji mkubwa, utakaowezesha kumudu upatikanaji na utoaji wa huduma bora kwa wageni wote kwa wakati kwa viwango vinavyokidhi matakwa ya wageni.

"Kwa sasa 'season' za utalii zinaungana, kila wakati tunapokea wageni wa ndani na nje ya nchi wakifika hapa kwa shughuli mbalimbali, wapo wanaokuja kwa mikutano na kutembelea vivutio vya utalii, lakini wapo wanaokuja kwa kutalii moja kwa moja na wote wanahitaji kupata huduma stahiki zinazokidhi mahitaji yao, tunahitaji kujipanga vema ili kumudu kuwahudumia bila kuelemewa na waondoke wakiwa wameridhishwa na huduma hizi". Amesema Mongela.

Aidha, amewataka wakazi wa mkoa huo kuwa tayari kupokea wageni wengi na kuendelea kuwasihi watu wote kuchangamkia fursa hiyo kujipatia vipato ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, wa mkoa kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mhe. Mongella amethibitisha kuwa Filamu ya Royal Tour iliyofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kupitia sekta ya utalii, ambayo ndio muhimili mama wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

"Kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Arusha, tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, ninamshukuru Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kufufua Utalii nchini sekta ambayo ilikumbwa na changamoto kubwa wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO 19.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi