Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Arusha DC yakabiliwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia
Nov 01, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Prisca Libaga - Arusha.

Halmashauri ya Arusha iliyoko Wilayani, Arumeru Mkoani hapa,inakabiliwa na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia,Mimba za Utotoni na ulawiti kwa watoto wadogo imeelezwa.

Hayo yalisemwa na Afisa Elimu wa Shule za Msingi wa halmashauri hiyo Tumsifu Mushi, wakati wa uwasilishaji wa taarifa za Kata katika kikao cha Baraza la Madiwani   uliofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo mwisho mwa wiki.

Alisema kuwa halmashauri hiyo pia inakabiliwa na tatizo la ndoa za utotoni ambapo takribani watoto 138 wamechumbiwa wakiwa shuleni wakati wakiendelea na Masomo kutokana na mila zilizopitwa na wakati. Mushi, alisema kuwa watoto 71 wanatoka katika shule ya msingi Engalaoni kata ya Mwandeti na wengine  67 wakitokea shule ya msingi Laroi kata ya Laroi ni wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.. Aliongeza kwa kusema kuwa baada ya kuzungumza na Baadhi ya watoto hao waliochumbiwa katika umri mdogo walisema kuwa siku ambazo hawaendi shuleni wazazi wao wanawaamuru kwenda kuwatembelea wachumba zao, na tayari kesi 16 zimeshafunguliwa dhidi ya watoto walioozwa katika umri mdogo.

Alisema kwamba katika suala la uandikishaji wa Wanafunzi wa Darasa la Kwanza Mwaka huu wameweza kuandikisha Wanafunzi kwa zaidi ya Asilimia 100, lakini bado kumekuwa na changamoto ya watoto wenye umri wa kwenda shule kutokuandikishwa na badala yake watoto hao wamekuwa wakitumikishwa na Wazazi wao katika Kazi za Majumbani. Amekiambia kikao hicho kwamba  Idara ya Elimu imefanya utafiti  kwenye kata ya Mwandeti  na kubaini kuwa  zaidi ya watoto 100 wenye umri wa kuandikishwa shule wanatumikishwa na wazazi wao katika shughuli ya kuchunga Mifugo  jambo ambalo limesababisha watoto hao kushindwa kwenda Shuleni. Afisa Elimu huyo alieleza Baraza la Madiwani kwamba  tatizo ni kubwa sana na linaathiri hata kiwango cha ufaulu  lakini  kwa sasa jamii imechukulia kuwa mwanafunzi akipata mimba hataruhusiwa kuendelea na masomo hivyo wanapewa mimba ili iwe rahisi kuwaoa. Akichangia kwenye kikao hicho Diwani wa kata ya Mwandeti  Boniface Tarakwa ,alisema  tatizo hilo lipo katika kata yake na changamoto iliyopo ipo kwenye  vyombo vya Sheria hasa katika masuala ya  mtoto kwani hata watuhumiwa akikamatwa na  kupelekwa Mahakamani hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. Amekiambia kikao hicho kwamba wanapowakamata watuhumiwa wa matukio hayo na wanapowafikisha  kwenye vyombo vya sheria baada ya muda mfupi  watuhumiwa wanarudi nyumbani, na huo ndio unaokuwa mwisho wa kesi hali hiyo inawachanganya. Diwani mmoja pia alitoa mfano kuwa mwaka jana wapo  wazazi na wanafunzi waliokamatwa kwa kutokuwapeleka watoto shuleni ambao waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na waliwachukulia hatua kwa kuwapelekwa Polisi na hawakujua kesi ilipoishia na Watuhumiwa walitoka na kuendelea na shughuli zao kama kawaida. Kwa upande wake Diwani wa kata ya Oldonyosambu Raymond Lairumbe alisema kuwa mila na desturi za jamii ya kimaasai  zimekuwa zikiathi mwenendo mzima wa mashauri yanayohusu ukatili dhidi ya watoto hivyo Mahakama kushindwa kupata ushahidi jambo linalosababisha kesi hizo kushindwa kuendelea.

Mwenyekiti wa halmshauri hiyo,  Noah Lembris alisiwasisitiza Madiwani kuhakikisha wanajipanga ipasavyo  kupiga vita ukatili wa Kijinsia wanapokuwa  kwenye vikao  vyao, na  wawaelimishe Wananchi madhara  yatokanayo na  ukatili kwa watoto.

Amewasisitiza madiwani kusimama imara kwa kuwashughulikia wale wote watakaojihusisha na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kukomesha tabia ya wahalifu kukimbilia kwao au viongozi wa mila kwa ajili ya kutafuta suluhu.

Pia aliwaasa baadhi ya madiwani na viongozi wa mila ambao wamekuwa wakiwakingia vifua wahalifu wanapofanya makosa hivyo akawaomba kuacha sheria ichukue mkondo wake ili kukomesha tabia hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi