Na Shamimu Nyaki- India
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.Pauline Gekul ameipongeza timu ya Taifa ya Wanawake chini ya Miaka 17 (Serengeti Girls) kwa ushindi wa magoli mawili kwa moja dhidi ya Ufaransa.
Mechi hiyo ya Kundi D iliyochezwa Oktoba 15, 2022 Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru jijini Goa, India imeipandisha Tanzania hadi nafasi ya pili nyuma ya Japan na mbele ya Canada na Ufaransa katika kundi hilo.
"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan inatoa mchango mkubwa kwa timu zinazowakilisha vyema nchi, na ndio maana hata nyie Serengeti Girls Serikali ipo hapa nanyi kuhakikisha inawaunga mkono mfanye vizuri," amesema Mhe. Gekul
Kwa upande wake Kocha wa timu, Bakari Shime amesema vijana wanaendelea kuimarika na kusahihisha makosa ya Mechi ya kwanza dhidi ya Japan ambayo leo umeleta matokeo mazuri.
" Kesho tutaelekea Mumbai na tukifika tutafanya mazoezi kwa ajili ya mchezo na Canada ambao tukishinda tunasonga mbele," amesema Kocha Shime.
Tanzania ipo katika kundi D pamoja na Japan, Ufaransa na Canada.