Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Anayevuruga Mitihani Ashitakiwe Mahakamani, Ahukumiwe na Aende jela-Waziri Mkenda 
Dec 05, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mathias Canal, WEST - Dar es salaam

Serikali imeweka bayana dhamira yake ya kuchukua hatua kali za uwajibikaji kwa Maafisa Elimu wa Mikoa, Wilaya, Walimu na maafisa wengine wote wakiwemo askari ambao wamepewa jukumu la kusimamia mitihani.

Hatua hizo dhidi ya wasimamizi hao wa mitihani zitahusisha kusimamishwa kazi, kufukuzwa pamoja na kufikishwa mahakamani ili wafungwe jela.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 5 Disemba, 2022 wakati akizungumza na uongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kampasi ya Mlongazila katika Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es salaam alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja.

Amesema kuwa ili kuimarisha sekta ya elimu lazima kushughulika na watu wanaofanya udanganyifu ikiwemo kuwachukulia hatua kali na kuwajibika huko sio tu kufukuzwa kazi kama ilivyozoeleka au kupewa onyo pekee bali wafungwe jela ili iwe fundisho kwa wengine.

Waziri Mkenda amesema kuwa Baraza la Mitihani Tanzania (NACTE) limeongeza mikakati ya kupambana na watu ambao wanafanya udanganyifu kwenye vituo vya mitihani ambapo serikali imewakamata na kuwachukulia hatua wasimamizi wote kwa kushirikiana kufanya ubadhilifu wa mitihani.

Amesema kuwa Serikali imechunguza na kubaini kuwa watumishi wa Serikali na watumishi wa sekta binafsi wamehusika kwenye udanganyifu wa elimu na kuwachukulia hatua.

"Sasa nisisitize kuna kauli inasema ukitaka kuuwa Taifa basi uwa elimu, sasa tunafanya mageuzi ya elimu nchini kwenye sera na mitaala lakini haiondoi jukumu la kusimamia elimu tunayoitoa sasa hivi inatolewa kwa taratibu zinazokubalika", amesisitiza Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda amesema kuwa udanganyifu katika mitihani una madhara ya kumuwezesha mtu kufaulu ambaye hakustahili kufaulu kwani akiwa Daktari ataleta athari kubwa katika jamii.

"Hasara mojawapo kubwa kwa Taifa letu ya kuvujisha mitihani ni kuwafundisha watoto katika umri mdogo kwamba ili uendelee ni lazima ufanye udanganyifu, tunaanza kujenga rushwa mapema mno na Serikali haitakubali kitu kama hicho", amekaririwa Waziri Mkenda

"Wale waliohusika hasa Watumishi wa Serikali, Maafisa elimu na watu wote waliohusika mahali pao kwa kweli ni jela, tunaongea na mamlaka husika kwamba tusije tukawafukuza tu kazi, wanachokifanya ni jinai, ukiangalia gharama za kuendesha mitihani ni kubwa sana kwa hiyo watu wanaovuruga mitihani washitakiwe mahakamani wahukumiwe na waende jela." Amesisitiza Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda ameeleza kuwa Serikali itapitia sheria ili kama kuna mwanya wa kuwawezesha watu kufanya udanganyifu na wakatoka bila kuchukuliwa hatua yoyote kuwe na namna ya kufanya mabadiliko.

Amesema anayechezea mtihani afungwe jela na ametoa onyo kwa wote wanaofanya hivyo kuacha mara moja udanganyifu huo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi