Na Mwandishi Wetu-DODOMA
Amani na utulivu vimetawala nchi nzima wakati watanzania wakijitokeza kupiga kura kuwachagua viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wawakilishi, Wabunge na Madiwani.
Jijini Dodoma, katika vituo mbalimbali vya kupigia kura vikiwemo Kilimani, Chang’ombe, Ipagala, Nzuguni, Kisasa na maeneo mengi ya Dodoma hali imeonekana kuwa yenye utulivu na wananchi wakipiga kura bila kuwa na msongamano au changamoto zenye kuathiri upigaji kura.
Shadrack Mwamba (38) wa Nzuguni, Dodoma ambaye amepigia kura katika Kituo cha Shule ya Msingi Nzuguni, anaipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa maandalizi mazuri na jinsi Wasimamizi wa uchaguzi wanavyotoa msaada kwa wananchi kuhakikisha wanapiga kura bila shida.
Jijini Dar es Salaam, Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Askofu Dkt. Alex Malasusa amepiga kura na kueleza kuridhishwa zoezi la upigaji kura. “Nimefurahishwa katika Vituo vya kupigia kura kulikuwa na watu wakusaidia kutambua jina lako na kikubwa zaidi ni kwamba watu wenye mahitaji maalumu wamehudumiwa kwa haraka”, ameeleza.
Amesema kuwa Mawakala wote wa Vyama wapo katika Vituo vya kupigia kura na kabla ya kupiga kura mtu anatoa kitambulisho na kuitwa jina kwa sauti ambapo kila mtu wakiwemo Mawakala wanasikia na hivyo kuweka uwazi katika zoezi zima.
“Nichukue fursa hii kumshukuru Mungu kwa kuwezesha kumalizika Kampeni kwa amani na pia amani inavyoendelea kutawala katika Vituo vya kupiga kura. Hii ni ishara kwamba amani itaendelea hata baada ya kuanza kutangazwa matokeo”, amesisitiza Dkt. Malasusa.
Bw. Mohamed Hassan wa Mbagala Rangi Tatu, Dar es Salaam anasema wananchi wa huko wameridhishwa na taratibu za upigaji kura yakiwemo maelekezo yanayotolewa na Wasimamizi wa Vituo vya kupigia kura.
“Uchaguzi wa mwaka huu una utulivu na amani, na nawasihi watanzania waendelee kujitokeza kwa wingi kuwapigia kura wagombea wanaowapenda. Wasismamizi wanatusaidia kuangalia majina yetu kupitia karatasi au hata kupitia simu ya mkononi na hivyo kurahisisha zoezi zima la upigaji kura”, anaeleza Bw. Mohamed.
Huko katika Jiji la Arusha, Bw. Sadiki Ismail (52) aliyepiga kura katika Kituo cha Shule ya Sekondari Kaloleni anasema zoezi linaenda vizuri tofauti na watu walivyokuwa wanafikiria.
“Kwa kweli tumefurahishwa na utaratibu unaoendelea katika Kituo hiki na maeneo mengine ya hapa Arusha. Tumepiga kura kwa amani na hakuna usumbufu wa ainayeyote ile”, ameeleza Bw. Ismail.