TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
ALIYEKUWA KARANI WA BARAZA LA MAWAZIRI AAGWA DAR
WAZIRI MKUU Mhe. Kassim Majaliwa ameungana na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, viongozi waandamizi wa Serikali na mamia ya wananchi kuuaga mwili wa aliyekuwa Karani wa Baraza la Mawaziri Bw. Hassan Shebuge.
Marehemu Bw. Shebuge ameagwa leo (Ijumaa, Julai 7, 2017) nyumbani kwake Mbagala Majimatitu Jijini Dar es Salaam na anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumamosi, Julai 8, 2017), katika kijiji cha Funta, Bumbuli mkoani Tanga.
Bw. Shebuge alifariki dunia jana (Alhamisi, Julai 6, 2017) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kupata na shinikizo la damu.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia, Waziri Mkuu amesema kifo hicho ni pigo kwa Serikali.
Amesema enzi za uhai wake marehemu Shebuge alikuwa mpole na muadilifu na kutoa mchango mkubwa kwenye kufanikisha maamuzi na utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa ufanisi.
“Kwa kweli hatuna budi kwa sasa wajibu wetu sote ni kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema.”
Awali, Katibu Mkuu Ikulu, Bw. Alphayo Kidata akisoma wasifu wa marehemu Shebuge, alisema marehemu alizaliwa Mei 25, 1969 wilayani Korogwe, Tanga.
Alisema marehemu alipata elimu ya msingi katika shule ya Mkwakwani kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1983, ambapo alipata elimu ya sekondari katika shule ya Usagara kuanzia mwaka 1984 hadi mwaka 1987, zote za mkoani Tanga.
Bw. Kidata alisema mwaka 1988, marehemu alijiunga na shule ya sekondari ya Ilboru mkoani Arusha kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na cha sita.
Alisema mwaka 1992 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kupata shahada ya Sanaa na Ustawi wa Jamii mwaka 1995, mwaka 1998 alipata shahada ya uzamili ya Sanaa na Ustawi wa jamii. Pia marehemu alipata mafunzo mengine mbalimbali ndani na nje ya nchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JULAI 07, 2017