Na. Georgina Misama
Katika hatua za kuunga mkono utendaji kazi wa Rais John Pombe Magufuli, Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) imesema imeanza kuchukua hatua za kuwawajibisha wafanyakazi wazembe na wasio waadilifu.
Akiongea na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO leo Jijini Dar nes Salaam, Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Bw. Gulamhafeez Mukadamu alisema kwamba ili kurejesha imani iliyopotea kwa Wanajumuiya wa ALAT, hatua mbalimbali za kinidhamu zitachukuliwa kwa baadhi ya watumishi wa ALAT Makao Makuu.
“Katika Mkutano wetu Mkuu wa Taifa wa 33, utakaofanyika Septemba 19, 2017, tutatoa taarifa ya hatua zinazochukuliwa na zitakazochuliwa kwa watumishi wa Sekretarieti ya ALAT Makao Makuu ambao siyo waadilifu na wenye utendaji kazi usioridhisha ili kuweka mwelekeo mpya wa ALAT,” alieleza Mukadamu.
Aidha, Mwenyekiti huyo alieleza kuwa, kwa kuona umuhimu wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano, ALAF inaunga mkono juhudi za Mhe. Rais za Serikali kuhamia Dodoma, ambapo kuanzia tarehe Mosi Agosti mwaka huu ALAT nayo itahamishia Makao Makuu ya ofisi zake Mjini Dodoma.
Bw. Mukadamu pia alitumia wasaa huo kutoa taarifa ya Mkutano Mkuu wa 33 wa Kawaida, unaotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu Jijini Mbeya na kuhudhuriwa na takribani wajumbe 500. Mkutano huo utahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Vitengo, Wakuu wa Taasisi za Serikali za Mitaa na Maofisa kutoka Sekretarieti za Mikoa.
Kwa Mujibu wa Mukadamu, mkutano huo pia utahudhuriwa na wawakilishi wa Wabia katika Maendeleo na Mabalozi, Jumuia za Serikali za Mitaa za nchi za Kenya (ALGAK), Uganda (ULGA) na Rwanda (ABELO) pamoja na Asasi zisizo za Serikali na Sekta binafsi.
Jumuia ya Tawala ya Mitaa Tanzania ilianzishwa Mjini Dodoma, Desemba 1984 baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa Serikali za Mitaa kwa lengo la kuwakilisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa inayoziunganisha Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya Tanzania Bara.