Serikali ya Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) ambapo wajumbe zaidi ya 3,000 wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wakiwemo Marais kutoka nchi mbalimbali Afrika, viongozi wa wakuu wa nchi, wageni mashuhuri na wataalam wa Sekta ya Kilimo na Mifugo.
Katika Mkutano huo, Tanzania inatarajiwa kutangaza fursa zilizopo kwenye Sekta ya Kilimo ambapo wageni kutoka nje watapitishwa kwenye maeneo mbalimbali ambayo ni vivutio vya uwekezaji kwenye kilimo.
Akizungumza leo Septemba 03, 2023 jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano Maalumu kati ya Mawaziri wa Kisekta na Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe alisema ratiba ya Mkutano huo itaanza tarehe 5/9/2023 na baadhi ya wageni walishafika nchi ili kutembezwa kwenye maeneo ya vivutio vya uwekezaji wa kilimo.
“Tutakapomaliza mkutano, mtashuhudia miradi ambayo imetokana na mkutano huu, wageni wengi wanaokuja ni ili wapate nafasi ya kuendeleza majadiliano ambayo tuliyaanza awali na kutembelea maeneo yenye mvuto wa uwekezaji katika kilimo kama vile Bagamoyo, Zanzibar, Morogoro na Mikoa ya Nyanda za juu ,” alisema Bashe.
Awali akitoa maneno ya utangulizi, Mkurugenzi wa Mawasilino ya Rais, Zuhura Yunus alisema wageni kutoka mataifa zaidi ya 70 watahudhuria mkutano huo ili kujadili, kubadilishana uzoefu, kutangaza utalii na fursa za biashara na uwekezaji zilizopo.
“Wageni wengine watakaohudhuria Mkutano huo ni Washirika 26 wanaochangia Maendeleo ya Kilimo barani Afrika ambao wamejikita katika kuimarisha mifumo ya usalama wa chakula, ustawi wa kiuchumi na uendelevu wa maliasili,” alisema Zuhura.