Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na watanzania waishio nchini Ivory Coast, Mazungumzo yaliyofanyika katika Jiji la Abidjan.
Akizungumza na Watanzania hao, Makamu wa Rais amewapongeza kwa jitihada wanazofanya za kuchangia maendeleo katika sekta mbalimbali nchini Tanzania na kuwahakikishia kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wa wana diaspora hao na itaendelea kuunga mkono jitihada wanazofanya.
Makamu wa Rais amewaasa Watanzania hao kuendelea kuitangaza vema Tanzania, kuvutia wawekezaji pamoja na wao kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini. Pia amewasihi kuendelea kusaidia kwa karibu ndugu na jamaa wenye uhitaji katika familia zao nchini Tanzania kwa kutumia mifumo rasmi ya utumaji kifedha.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema kutokana na lugha ya Kiswahili kuanza kutumika katika Jumuiya mbalimbali kama lugha rasmi, Diaspora wanapaswa kuendeleza lugha hiyo kwa kuitangaza na kuanzisha vituo vya kujifunzia lugha ya Kiswahili katika maeneo waliyopo. Makamu wa Rais amesema suala la utangazaji wa lugha ya Kiswahili linapaswa kwenda sambamba na kutangaza utamaduni wa taifa la Tanzania pamoja na vivutio vizuri vilivyopo.
Makamu wa Rais amewataka Watanzania waishio nje ya Tanzania kutambua jukumu la kwanza la ujenzi wa Tanzania litafanywa na watanzania wenyewe hivyo wanapaswa kutoa mchango wa kila hali katika kuliletea taifa maendeleo.
Amesema Serikali itaendelea kuleta mabadiliko yenye tija kwa watanzania wote ikiwemo kuboresha sekta mbalimbali kama vile Afya , Elimu na Miundombinu pamoja na kueleza kwamba serikali inafanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha watanzania wanapata nafasi katika jumuiya na mashirika ya kimataifa ili kuwa na ujuzi utaoweza kulisaidia taifa.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk, Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Omar Said Shaban pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria anayewakilisha Tanzania Ivory Coast, Dkt. Benson Bana.
Makamu wa Rais yupo nchini Ivory Coast kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika kwa mwaka 2022 linalofanyika jijini Abidjan.