Na WMJJWM, Babati Manyara
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula ameitaka jamii kuzingatia malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili kuwa na watoto ambao watanajitambua na hatimaye kujenga kizazi kitakachokuwa cha mfano kwa ustawi wa Jamii.
Dkt. Chaula ameyasema hayo wilayani Babati mkoani Manyara wakati alipotembelea Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa huo kwa lengo la kukagua huduma zinazotolewa katika Makazi ya Wazee Magugu.
Dkt. Chaula ameongeza kuwa malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili kuwa na watoto ni muhimu kwa mtoto kwani yanamsadia mtoto kukua katika uelewa na kujiamini vitu ambavyo vitamuwezesha kuishi vizuri na jamii na kulea familia zao wakiwemo wazee.
"Sisi tuwe mfano tuwalee watoto wetu wajifunze kwetu ili hata tukizeeka na wao watatulea kwa sababu na sisi tuliwalea vizuri wakiwa Watoto", alisema Dkt. Chaula
Amesisitiza kuwa matatizo ya Wazee kutekelezwa na kutopata huduma kwa jamii ni matokea ya malezi waliowapa watoto wao, hivyo kusababisha watoto hao kutoona umuhimu wa malezi katika familia hasa kwa watoto na wazee.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Manyara, Karolina Mthapula alisema Mkoa utaendelea kushirikiana na Wizara katika kuhakikisha wazee wanapata huduma bora zaidi hasa wazee wasiojiweza katika kupata huduma za chakula na afya kwa ustawi wao.
Ameongeza kuwa mkoa unaendelea pia na kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto hasa tatizo la ukeketaji unaoendelea katika jamii kwa kuweka mikakati mbalimbali hasa kutoa elimu kwa jamii kuachana na vitendo hivyo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Afisa kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ziada Nkinda alisema Ofisi hiyo itaendelea kusimamia utoaji huduma bora kwa wazee hasa huduma za Afya kwa kuhakikisha wanapata huduma bora katika Vituo vya kutolea huduma za Afya nchini.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri wa Wazee Taifa, Mzee Lameck Sendo ameiomba jamii kuachana na imani pototu dhidi ya Wazee hasa kwa vijana kuona Wazee hawana umuhimu hivyo kutaka kuwaua na kurithi mali bali wawalee na kuwatunza wazee wao kwani ni tunu katika jamii na taifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula yupo katika ziara ya kikazi kukagua huduma zinazotolewa kwenye Makazi ya Wazee yaliyo chini ya Wizara hiyo.