Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Imeweka Mikakati Endelevu Upatikanaji Dawa
May 03, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Husna Saidi & Nuru Juma

Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeweka mikakati endelevu ya kuboresha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vyote vya huduma za afya nchini.

Hayo yamebainishwa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamis Adrea Kigwangalla akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa viti maalum Oliver Daniel Simguruka kuhusu hali ya upatikanaji wa dawa nchini katika kikao cha saba cha Bunge.

Dkt. Kigwangalla alisema kuwa hali ya upatikanaji wa dawa nchini umeimarika kwa asilimia 83 hivyo kufanya huduma hiyo ya afya kuwa bora.

“Hadi kufikia Aprili 2017 jumla ya shilingi bil.112 mil.198, 920,456 zimeshatolewa na kupelekwa kwenye bohari ya dawa ili kuwezesha vituo vya huduma za afya vya umma kupata mahitaji ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi”, alisema Dkt. Kigwangalla.

Aidha, alisema ongezeko hilo la fedha limesaidia kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya tofauti na miaka iliyopita.

Aliongeza kuwa hadi kufikia Januari 15 mwaka huu Mkoa wa Kagera pekee ulipokea kiasi cha shilingi bil.4 mil.150, 767,216 kupitia fungu namba 52 kutoka kwa Wizara hiyo ili kuboresha huduma ya afya Mkoani humo.

Akizungumzia ujenzi wa bohari za dawa katika kila kanda Dkt. Kigwangalla alisema kuwa Serikali imeendelea kuitatua changamoto hiyo baada ya hapo awali kukabiliwa na changamoto ya fedha katika kujenga bohari za dawa kila kanda.

Kwa upande mwingine aliwaomba viongozi wa ngazi zote waweze kushirikiana katika kudhibiti wizi wa dawa katika vituo vya huduma za afya kwa sababu hili ni jukumu la kila mmoja na pia alitoa wito kwa wananchi kuweza kutoa taarifa za wizi wa dawa ili sheria iweze kuchukuliwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi