Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

5G Kuimarisha Huduma za Biashara Mitandao
Aug 10, 2023
5G Kuimarisha Huduma za Biashara Mitandao
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria uzinduzi wa Mtandao wenye kasi ya 5G wa Kampuni ya Airtel Tanzania katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mkongo wa Mawasiliano Baharini cha Kampuni ya Airtel Tanzania kilichopo Mbezi Tanki Bovu Jijini Dar es Salaam tarehe 10 Agosti, 2023.
Na Lilian Lundo - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema huduma ya intaneti ya kasi ya 5G ambayo ameizindua leo Agosti 10, 2023 jijini Dar es Salaam itaimarisha utoaji wa huduma za biashara mtandao hapa nchini.

Mhe. Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa mkongo mkubwa wa mawasiliano wa baharini wa 2Afrika na huduma ya intaneti ya kazi ya 5G ya Airtel Tanzania.

“Mifumo hii imerahisisha sana utoaji wa huduma mbalimbali ikiwemo utunzaji taarifa muhimu, ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kutumia na kupokea fedha na taarifa pamoja na biashara za mitandao,” amesema Mhe. Rais.

Ameendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea na jitihada za kukuza matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa lengo la kujenga uchumi jumuishi wa kidigitali na kuboredha maisha ya wananchi wa mijini na vijijini.

Aidha amesema kuwa, kutokana na umuhimu wa TEHAMA hasa wakati huu ambao teknolojia inaendelea kukua kwa kwa kasi Serikali ya Awamu ya Sita imejizatiti kuweka mazingira wezeshi kwa kutoa huduma za wawekezaji na kujenga miundombinu ya mawasiliano.

“Hivi karibuni tumeanza mradi wa ujenzi wa minara mipya 758 kwa ajili ya kupanua wigo wa mawasiliano, ambapo utawanufaisha zaidi ya Watanzania Milioni 8 kote nchini mijini na vijijini,” amefafanua Mhe. Rais.

Mhe. Rais ametoa agizo kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambayo inasimamia sera ya TEHAMA, pamoja na wizara nyingine na taasisi husika kuhakikisha mifumo yote ya TEHAMA inayotumika ndani ya Serikali inasomana.

Vilevile ametoa wito kwa watoa huduma ndani ya Tanzania, mabenki, Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya ambazo zinatoa huduma, kuwa na namba moja ambayo itamtambulisha Mtanzania katika kila huduma atakayokuwa anaitumia kuanzia siku anayozaliwa.

Mhe. Rais amesema kuwa, kupitia namba hiyo itawezesha kumjua kila Mtanzania.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo amewakaribisha wawekezaji wengi zaidi kuja kuwekeza Tanzania, kama ambavyo Airtel walivyoleta teknolojia mpya nchini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi