WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Sera, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, (pichani), ameziagiza taasisi za umma na binafsi nchini zinapotoa fedha za kusaidia jamii (CSR), zikumbuke kuna kundi maalum la walemavu nchini ambao nao wanahitaji huduma maalum kama wanavyohitaji wengine.
Mheshimiwa Waziri aliyasema hayo jioni ya Septemba 17, 2018 wakati akipokea mashine maalum za kuandika kwa wanafunzi wasioona (Braille Machines) kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwenye chuo cha walemavu Yombo jijini Dar es Salaam.
“Tunapoona kwenye shule za msingi wanahitaji madawati, tukumbuke kwamba, wapo wanafunzi kwenye vyuo, wapo wanafunzi kwenye shule za msingi, ambao ni wenye ulemavu ambao pengine badala ya madawati, wao wanahitaji viti vya kuwaongezea mwendo, au kama tunatoa computer mpakato, tukumbuke kwamba tunazo shule na vyuo watoto wetu, vijana wetu wanasoma wenye ulemavu wangehitaji mashine hizi zenye kuandika nukta nundu ili kuwasaidia wenye ulemavu ili na wao wafaidike na elimu katika nchi yetu ya Tanzania.” Alisema Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama wakati akihutubia kwenye hafla ya kukabidhi mashine hizo.
Alisema, Amefarijika kuona maagizo ya Ofsii ya Waziri Mkuu, yameweza kutekelezwa na taasisi ambayo iko chini ya ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kusaidia kundi hilo la wenye ulemavu.“Vifaa nitakavyovikabidhi leo ni maalum kwa wenzetu wasioona na ni vya wanafunzi walioko katika vyuo mbalimbali kwenye nchi yetu siyo hapa Yombo peke yake.” Alifafanua.
Aliupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa msaada huo mkubwa na kwamba fedha walizotumia kununua vifaa hivyo ni kuwekeza kwa vijana ili kujiandaa kuwa na utashi na weledi na kujiandaa kuingia kwenye soko la ajira nchini.
Akimkaribisha Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu, Mhe. Stella Ikupa, ameitaka jamii ya watu wenye ulemavu nchini kujiamini, kujitambua, kujikubali na kuongeza bidii katika kazi wanazofanya.“Kama ni mwanafunzi weka bidii katika masomo, na kama ni mwajiriwa weka bidii katika kazi yako kwani huo ndio ukombozi kwa mtu mwenye ulemavu.” Alisema Mhe. Ikupa.
Alisema vifaa vilivyopokelewa ni muhimu sana kwa watu wenye ulemavu hususan kwa kundi la wasioona, kwani vitawawezesha katika dhana nzima ya ujumuishwaji mtu mwenye ulemavu anapopatiwa vifaa vinavyoweza kutekeleza majukumu yake anakuwa anawezeshwa kuwa katika ujumuishwaji kwa hiyo atajumuishwa katika elimu lakini hatimaye atajikuta amefikia kwenye eneo la ajira na hatimaye kujikomboa na kuon dokana na utegemezi na uombaomba.“Nikiwa kama Naibu Waziri ninayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, nitoe pongezi za kipekee kwa uongozi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa tendo hili kubwa ambalo mmelifanya.” Alipongeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF) Bw. Masha Mshomba alisema, Mwaka jana (2017) WCF ilifanya Mkutano wa kwanza wa mwaka na katika mkutano ule Mfuko uliahidi kupitia mpango wake wa kusaidia jamii (CSR) utasaidia watu wenye ulemavu na kwamba ahadi hiyo imetekelezwa.
“Tumetoa msada wa mashine hizi maalum (Braille Machines) 13 zenye thamani ya Shilinhgi Milioni 33.8 na tunaimani kwamba zitawasaidia sana wenzetu wasioona ili kuwafanya washiriki kwa ufanisi katika kujifunza.” Alisema.
Alisema, Sekta ya Hifadhi ya Jamii, WCF ikiwa ni miongoni mwa sekta hiyo, moja ya majukumu ambayo serikali inasisitiza ni kuhakikisha ushiriki wa sekta katika kuondoa changamoto kwenye makundi maalum na hatua hiyo ya kutoa msada ni utekelezaji wa maagizo hayo ya serikali.
Katika awamu hii ya kwanza taasisi zilizofaidika ni pamoja na Chuo cha Ufundi kwa Walemavu Yombo Dar es Salaam na Sabasaba kilichoko Singida, Shule za Uhuru Mchanganyiko ya Dar es Salaam, Shule ya Msingi Ndanda, iliyoko Mkoani Mtwara, Shule ya msingi Biharamulo, Shule ya Msingi Mgeta Mseto iliyoko Bukoba Mkoani Kagera.