Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Aug 31, 2018
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wote nchini kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria sambamba na kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi ya wananchi.

Mhe. Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo tarehe 30 Agosti, 2018 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, wakati akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa wilaya hiyo, ambapo amesisitiza kuwa viongozi wote wajenge utaratibu wa kusoma sheria na kujiepusha kutumiwa kwa maslahi ya watu binafsi.

Huku akitolea mfano wa mgogoro wa makontena yanayodaiwa kuwa na fenicha za shule, na yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika bandari ya Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli amesema makontena hayo yanapaswa kulipiwa kodi kwa mujibu wa sheria, huku akisisitiza kuwa Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye dhamana ya kupokea misaada kwa niaba ya Serikali na sio Mkuu wa Mkoa.

Kwa mujibu wa sheria ya Madeni, Dhamana na Misaada Namba 30 ya mwaka 1974 (kama ilivyorekebishwa na sheria namba 9 ya mwaka 2003) kifungu cha 3, 6, 13 na 15, Waziri wa Fedha na Mipango ndiye mwenye mamlaka ya kukopa nje na ndani, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali.

“Kwa msingi huo, hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kukopa, kutoa dhamana na kupokea misaada kwa niaba ya Serikali bila mtu huyo kukasimiwa mamlaka hayo na Waziri wa Fedha kwa mujibu wa sheria hiyo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka Madiwani wa halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha wanasimamia kwa ukaribu matumizi ya fedha za bajeti ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha hizo zinaelekezwa katika miradi na huduma zenye kujibu kero na kuboresha maisha ya wananchi badala ya kuacha zikitumiwa kulipana posho za vikao na safari zisizo na tija.

“Nafahamu kuwa hata nyie Madiwani huwa mnakaa kikao siku moja na mnataka kulipwa posho ya siku mbili au tatu, au mtumishi wa halmashauri anasafiri kwa siku mbili lakini anaandikiwa posho za siku nne, nataka mchezo huu ukome, elekezeni fedha kwenye mahitaji muhimu ya wananchi, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya simamieni hilo” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Katika mkutano huo ambapo alianza kwa kupokea maswali, kero na maoni ya wafanyakazi na viongozi, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa kujitegemea na kutatua kero za wananchi wakiwemo wafanyakazi wote bila kubagua na amewataka viongozi wa Wilaya ya Chato kuwa wabunifu wa namna ya kuharakisha maendeleo ya wananchi badala ya kubweteka kwa kutegemea kupendelewa naye kwa kigezo cha kuwa mwananchi wa Chato.

“Mimi ni Rais wa Tanzania nzima sio Rais wa Chato, nina wajibu wa kuhudumia Tanzania nzima, kwa hiyo mambo ya hapa Chato wabaneni viongozi wa hapa Chato” amebainisha Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu uhaba wa watumishi, Mhe. Rais Magufuli amesema baada ya Serikali kuokoa Shilingi Bilioni 138 zilizokuwa zikilipwa kwa watumishi hewa na wenye vyeti feki, sasa imeanza kuajiri watumishi ambapo watumishi 52,000 wanaajiriwa na kwamba sambamba na hilo katika kipindi kifupi kijacho itaanza kulipa madeni ya watumishi baada ya uhakiki kukamilika.

Amewaagiza viongozi wa wilaya ya Chato ambao wamesikiliza kero za wafanyakazi na Madiwani akiwemo Mbunge wa Jimbo hilo na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani kufanyia kazi kero zote zilizo ndani ya uwezo wao.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Chato, Geita

30 Agosti, 2018

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi