Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waweka Hazina, Wahasibu Watakiwa Kuzingatiai Matumizi Sahihi ya Fedha
Jun 11, 2018
Na Msemaji Mkuu

Mkurugenzi Msaidizi TEHAMA, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Bartazal Kibola akifungua mafunzo ya mfumo wa malipo (epicor 10.2) kwa Waweka Hazina na Wahasibu (hawapo pichani)  kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha na Manyara, leo Jijini Dodoma

Na:  Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.     

Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha zinazotumwa katika Halmashauri zao.

Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi TEHAMA, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Bartazal Kibola alipokuwa akifungua mafunzo ya mfumo wa malipo (epicor 10.2) kwa Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha na Manyara. Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Wahasibu hao namna ya kutumia mfumo huo ambao umeboreshwa zaidi.

“Mfumo huu mpya utakapoanza kutumika lazima sheria na taratibu zifuatwe, matumizi ya fedha yaendane na bajeti ya Halmashauri husika, vilevile ni muhimu kuhakikisha kuwa vifungu vyenu vya fedha vinakaa vizuri,” alisema Kibola.

Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bibi Beatrice Kimoleta akitoa maelekezo ya mafunzo ya mfumo wa epicor 10.2 kwa Waweka Hazina na Wahasibu (hawapo pichani) kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha na Manyara, leo Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendelea jijini humo.

Aliendelea kusema, mfumo huo umerahisha kazi na kupunguza gharama ambapo mabadiliko yote ya bajeti yatakuwa yakifanyika kupitia mfumo huo tofauti na ilivyokuwa awali ambapo Halmashauri zililazimika kutuma barua za mabadiliko ya bajeti ofisi za TAMISEMI.

Aidha,  amesema mfumo huo utatatua baadhi ya changamoto zilizokuwepo katika mfumo uliopita epicor toleo Na. 9.05  ikiwa ni pamoja na changamoto ya kutoa taarifa za utekelezaji mara baada ya kufanya matumizi kwa kuzingatia mipango iliyojiwekea Halmashauri husika.

Hivyo basi epicor toleo namba 10.2 itaondoa kabisa tatizo la taarifa hizo kwani mfumo huo baada ya malipo kufanyika utakuwa na uwezo wa kupeleka taarifa hizo kwenye mfumo wa mipango na bajeti ambapo pia mfumo wa FFARS utakuwa umepokea taarifa hizo za matumizi ya vituo na hivyo taarifa zote za  utekelezaji kupatikana moja kwa moja kutoka mfumo wa Plan Rep ambao pia umeunganishwa na mfumo wa epicor 10.2.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais, TAMISEMI Bibi Beatrice Kimoleta amewataka Wahasibu hao kuingiza takwimu sahihi katika mfumo huo ili mfumo uweze kuongea taarifa ambazo ni sahihi.

Meneja  wa Mradi wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) Mkoani Dodoma,  Bw.  Gideon Muganda akitoa maelekezo kuhusu ushiriki wa PS3 katika mfumo wa malipo (epicor 10.2) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya mfumo huo kwa Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha na Manyara, leo Jijini Dodoma.

Vile vile, ameshukuru Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (Ps3) kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kwa kuwezesha uboreshaji wa mfumo huo ambao utaleta uwazi katika mapato na matumizi ya fedha za Umma katika Halmashauri zote hapa nchini.

Mfumo wa malipo (epicor 10.2) unatarajiwa kuanza kutumika katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini kuanzia Julai 1 mwaka huu. Mfumo huo utahusisha masuala yote ya fedha za Mamlaka hizo ikiwa ni pamoja na mapato, matumizi pamoja na bajeti nzima ya Mamlaka husika.

Waweka Hazina na Wahasibu kutoka Halmashauri za Mikoa ya Arusha na Manyara wakimsikiliza mgeni rasmi Mkurugenzi Msaidizi TEHAMA, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Bartazal Kibola (aliyesimama) ambaye alifungua mafunzo ya mfumo wa malipo (epicor 10.2) kwa niaba ya Mkurugenzi wa TEHAMA, Ofisi Rais TAMISEMI, leo Jijini. Waweka Hazina na Wahasibu kutokana Mamlaka za zote za Serikali za Mitaa wanajengewa uwezo wa kutumia mfumo huo utakaohusisha masuala yote ya fedha ikiwemo mapato, matumizi pamoja na bajeti za Halmashauri husika. Mfumo huo utaanza kutumika rasmi Julai 1, mwaka huu.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi