Wagonjwa 15 Wafanyiwa Upasuaji wa Kupandikiza Mishipa ya Damu Katika Moyo na Kurekebisha Mshipa Mkubwa wa Damu Katika Kambi Maalum ya Matibabu
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Saifee ya Mjini Mumbai nchini India wamefanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa wagonjwa 15 katika kambi maalum ya upasuaji ya siku sita inayomalizika kesho.
Upasuaji wa moyo unaofanyika katika kambi hii ambayo imeanza Jumatatu tarehe 8/11/2017 hadi Jumamosi tarehe 11/11/2017 ni ya upasuaji wa kufungua kifua kwa watu wazima. Upasuaji uliofanyika ni wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (CABG – Coronary Artery Bypass Grafting), na kubadili milango miwili hadi mitatu ya moyo (Valve Replacement).
Kwa mara ya kwanza hapa nchini tumefanya upasuaji wa kurekebisa mshipa mkubwa unaotoa damu kwenye moyo kwenda sehemu zote za mwili (Aortic Aneurysm Repair).
Tulifanya upasuaji kwa wagonjwa watatu kwa siku, wote hawa wanaendelea vizuri na wataruhusiwa pindi afya zao zitakapoimarika. Baadhi yao ambao tumewafanyia upasuaji jana na juzi wako katika chumba cha uangalizi maalum na wengine wako wodini wameshaanza kufanya mazoezi.
Kama wagonjwa hawa wangeenda kutibiwa nje ya nchi Serikali ingelipia zaidi ya milioni 405 kwani gharama za mgonjwa mmoja kwenda kutibiwa nje ya nchi ni zaidi ya milioni 27. Gharama za matibabu haya hapa nchini kwa wagonjwa 15 ni milioni 225 (milioni 15 kwa mgonjwa mmoja).
Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo katika matibabu ya wagonjwa wetu ni wagonjwa wengi tunaowapokea mioyo yao kutokuwa katika hali nzuri. Tunawashauri wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara hii itawasaidia kujuwa kama wana matatizo ya moyo au la na hivyo kupata tiba kwa wakati.
Kama mnavyofahamu matibabu ya moyo ni ya gharama hivyo basi tunaendelea kuwahimiza wananchi kujiunga na mfuko wa taifa wa bima ya afya ambao utawasaidia kulipa gharama za matibabu pindi watakapougua na kuhitaji kupata matibabu.
Kwa namna ya kipekee Taasisi inaishukuru Hospitali ya Seifee kutokana na ushirikianao mzuri tuliokuwa nao, licha ya kutoa matibabu kwa wagonjwa tumekuwa tukibadilishana ujuzi wa kazi wakati wa kufanya upasuaji. Kwa mwaka huu hii ni mara ya pili kwa wataalamu hawa kuja katika Taasisi yetu. Mwezi wa tatu mwishoni tulifanya nao kambi ya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa nane (8).
Aidha tunatarajia kuwa na kambi maalum ya matibabu ya moyo ya bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo maalum wa Cathlab kwa watu wazima itakayoanza tarehe 14/11/2017 hadi tarehe 19/11/2017. Katika kambi hii ambayo tutashirikiana na wenzetu kutoka Taasisi ya Sharjah Charity kutoka Falme za Kiarabu tunatarajia kufanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 50.
Tunawaomba wananchi waendeleee kuchangia damu kwani wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji wa moyo wanahitaji kuongezewa damu wakati wanapatiwa matibabu.Mgonjwa mmoja anahitaji damu kati ya chupa 5 hadi 6.
Kwa mtu mmoja mmoja au kikundi cha watu ambao wanapenda kuchangia damu tunawaomba wafike Taasisi ya Moyo iliyopo Muhimbili mkabala na Maabara kuu. Kwa maelezo zaidi wawasiliane kwa simu namba 022-2151379 au 0713304149.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano na Masoko
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
10/11/2017