Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wizara ya Nishati Yawanoa Wabunge
Sep 09, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_35041" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (aliyesimama), akizungumza wakati wa semina iliyoandaliwa na Wizara kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu masuala ya umeme, mafuta na gesi, jana Septemba 8, 2018 jijini Dodoma. Wengine pichani (Meza Kuu) kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Mwenyekiti wa Kamati Dustan Kitandula na Katibu wa Kamati Felister Mgonja.[/caption]

Na Veronica Simba  - Dodoma

Wizara ya Nishati imeandaa na kuendesha semina maalum kwa wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu masuala ya umeme, mafuta pamoja na gesi asilia.

Semina hiyo ya siku mbili ilifunguliwa rasmi jana, Septemba 8 2018 na Mwenyekiti wa Kamati, Dustan Kitandula katika Ukumbi wa Chuo cha VETA jijini Dodoma.

Akitoa muhtasari wa kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani aliiambia Kamati hiyo kuwa hali ya umeme nchini imeimarika kwa kiasi kikubwa.

“Hivi sasa tuna uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 1522 za umeme, ambapo ukijumlisha na nyingine 40 zilizoingia wiki iliyopita tunafikia megawati 1562 wakati matumizi yetu kwa siku mara nyingi ni megawati 920, hivyo tunabakiwa na ziada.”

Mbali na uzalishaji, Waziri Kalemani alitaja sababu nyingine iliyochangia kuimarisha huduma ya umeme nchini kuwa ni ujengaji wa njia za kusafirisha umeme mkubwa katika takribani kona kuu zote tatu za nchi hali ambayo ni tofauti na miaka mitatu iliyopita.

Akifafanua zaidi, Waziri alitaja njia za kusafirisha umeme mkubwa zilizojengwa katika maeneo mbalimbali nchini kuwa ni pamoja na ya Iringa hadi Mwanza yenye umeme wa kilovoti 400 na umbali wa kilomita 670. Nyingine, ni ya umeme wa kilovoti 132 inayotoka Dar es Salaam hadi Tanga, ya Dar es Salaam hadi Mtwara na pia ya Mwanza hadi Kagera.

“Hayo ni maendeleo makubwa sana, ndiyo maana mnaona kwa sasa umeme haukatiki-katiki. Unapokatika ni pale tunapokuwa tunafanya marekebisho katika eneo husika,” alisisitiza.

Aidha, Waziri Kalemani alieleza kuwa, sababu nyingine ya mafanikio yaliyofikiwa ni kuendelea kuunganisha katika Gridi ya Taifa, maeneo ambayo yalikuwa yakitumia umeme unaozalishwa kutumia mitambo ya mafuta ya dizeli, ambao ni wa gharama kubwa.

Mathalani, alisema kuwa Serikali itaokoa kiasi cha shilingi bilioni 1.9 kwa mwaka baada ya kuondoa mitambo mitano inayotumia umeme wa mafuta na kuunganisha Gridi ya Taifa umbali wa kilomita 250 kutoka Makambako mpaka Songea Mjini, na kuunga Wilaya zote za Mikoa ya Njombe na Ruvuma.

Alisema kazi hii inafanyika kupitia Mradi wa Makambako – Songea wenye umeme wa kilovoti 220, ambao tayari umekamilika na unatarajiwa kuunganisha Gridi mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba.

Waziri alitaja sehemu nyingine ambako mitambo ya kuzalisha umeme unaotokana na mafuta imezimwa baada ya kuunganishwa katika Gridi ya Taifa kuwa ni pamoja na Wilaya za Ngara, Biharamulo na Muleba mkoani Kagera. Aidha, alisema Serikali imeondoa Vituo mbalimbali vya kuzalisha umeme wa mafuta ikiwemo Aggreko, IPTL pamoja na Symbion; ambavyo vilikuwa vikitumia gharama kubwa.

Vilevile, Waziri alieleza kuwa amri ya Serikali kusitisha uagizaji wa nguzo za umeme nje ya nchi na kutumia zinazozalishwa ndani ya nchi umekuwa wenye manufaa makubwa.

Akieleza mojawapo ya faida kubwa iliyotokana na zuio hilo, Waziri Kalemani alisema kuwa imepunguza kwa asilimia kubwa idadi ya wateja waliokuwa wakisubiri huduma ya kuunganishiwa umeme kwa muda mrefu hadi kufikia mwaka mzima kutokana na uagizaji nje wa nguzo kutumia muda mrefu.

“Hali imebadilika sana sasa ambapo tumebakiwa na wateja 8500 tu nchi nzima wanaosubiri kuunganishiwa umeme kutoka jumla ya wateja 27,000 waliokuwa wanasubiria nguzo ili kuunganishwa tuliokuwa nao kufikia mwezi Mei mwaka huu.”

Kwa upande wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Waziri Kalemani alimpongeza Mkurugenzi wake Mkuu, Mhandisi Amos Maganga na Taasisi kwa ujumla kwa kuongeza jumla ya vijiji 1541 katika vile vilivyokuwa kwenye Mpango wa kuunganishiwa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu. Alisema kuwa, hilo limefanyika ili kukidhi mahitaji ya wananchi, hususan walioko katika vijiji ambavyo awali vilirukwa kwa bahati mbaya.

Akizungumzia kuhusu Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Waziri aliieleza Kamati kuwa, Shirika hilo limekwishaanza kufanya biashara kama ilivyokusudiwa ambapo baadhi ya wateja wakubwa wameanza kununua gesi asilia ikiwemo kampuni ya saruji ya Dangote.

Waziri Kalemani pia alizungumzia utendaji kazi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPBA) ulio chini ya Wizara, ambapo alisema umekuwa wenye tija kwa Taifa kwa kuhakikisha upatikanaji wa mafiuta ya kutosha pamoja na ubora wake.

Akitoa takwimu kuhusu upatikanaji wa mafuta ya kutosha nchini chini ya uratibu wa Wakala huo, Waziri alisema  hivi sasa nchi ina uwezo wa kuhifadhi mafuta ya ziada kwa hadi siku 35 kwa dizeli (lita 147,000), petroli kwa siku 28 hadi 37 (lita 98,000), mafuta ya taa kwa siku 27 hadi 28 (lita 6,000) na mafuta ya ndege (lita 12,000)

Pia, Waziri aliwaeleza wabunge kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), ambao pia uko chini ya Wizara kuwa ni kushughulikia utafutaji na uendelezaji wa rasilimali ya mafuta nchini; jukumu ambalo lilikuwa likifanywa na TPDC kabla ya kuondolewa kuwa shirika la umma na kutakiwa kufanya kazi kibiashara.

Vingozi wengine wa Serikali walioshiriki semina hiyo ni pamoja na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Wakuu wa Idara mbalimbali za Wizara, Wenyeviti wa Bodi za Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Watendaji/Wakurugenzi Wakuu wa Taasisi hizo pamoja na maafisa waandamizi kutoka wizarani na katika Taasisi husika.

Seina hiyo inatarajiwa kuhitimishwa leo, Septemba 9 2018 kwa majadiliano, maoni na melekezo kutoka kwa Kamati ya Bunge.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi