Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Miradi 8,058 ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira Yafanyiwa Mapitio
Mar 24, 2025
Miradi 8,058 ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira Yafanyiwa Mapitio
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Semesi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 24, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesajili na kufanya mapitio ya awali kwa miradi ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) 8,058 kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025.

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo, Dkt. Immaculate Semesi amesema hayo leo Machi 24, 2025 katika Ofisi za Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya baraza hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

“Kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, Baraza limefanikiwa kusajili na kufanya mapitio ya awali kwa miradi ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) 8,058, kati ya miradi hiyo, 5,784 ni ya TAM na 2,274 ni ya Ukaguzi wa Mazingira,” amefafanua Dkt. Immaculate.

Ameendelea kusema kuwa, jumla ya vikao 3,836 vya wataalam vilifanyika kwa ajili ya kufanya mapitio ya taarifa za TAM na ukaguzi wa miradi na kutoa mapendekezo ya maboresho na masuala ya msingi ya kuzingatiwa katiza taarifa hizo.

Aidha, miradi 4,570 iliidhinishwa na kupewa vyeti vya mazingira, ambapo vyeti 3,058 ni vya TAM, vyeti 765 vya ukaguzi, vyeti vya kubadili masharti 169, vyeti vilivyohamishwa umiliki 552, vyeti vya muda (PEC) 53 na cheti kilichorudishwa (certificate of surrender) 1.

Dkt. Immaculate ameongeza kuwa, baraza hilo limesajili wataalam elekezi wa mazingira 1,023 na kutoa vyeti vya utendaji kwa wataalam elekezi 503 baada ya kukidhi vigezo kwa mujibu wa Kanuni za Usajili na Utendaji wa wataalam elekezi wa mazingira za mwaka 2021.

“Usajili wa Wataalam Elekezi wa Mazingira unafanyika kupitia mfumo wa kielektroniki ambao umeongeza ufanisi wa kushughulikia maombi huku changamoto kubwa ikiwa ni waombaji wengi kukosa vigezo kutokana na kutokuelewa kanuni au kutokuwa makini wakati wa kuwasilisha maombi,” amefafanua Dkt. Immaculate.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi