Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

COSOTA Ilivyowanufaisha Wasanii Ndani ya Awamu ya Sita
Mar 21, 2025
COSOTA Ilivyowanufaisha Wasanii Ndani ya Awamu ya Sita
Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki (COSOTA), Bi. Doreen Sinare akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 21, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Adelina Johnbosco

Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA), Bi. Doreen Sinare, amesema ndani ya kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, COSOTA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na yamefanyika mambo mengi yaliyosaidia kuimarisha usimamizi wa hakimiliki kwa kazi za Sanaa na bunifu mbalimbali zinazolindwa na Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya Tanzania.

Bi. Sinare amebainisha hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Ofisi ya Hakimiliki Tanzania katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 21, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Jijini Dodoma.

“Kati ya mambo yaliyofanyika ni pamoja na marekebisho katika Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki Na. 7 ya mwaka 1999 yaliyofanyika kupitia Sheria ya Fedha katika mwaka 2022 na 2023. Mabadiliko haya makubwa yalianzisha chanzo kipya cha mapato cha tozo ya hakimiliki ambapo vifaa vinavyotumika kusambaza, kuzalisha na kuhifadhi kazi za sanaa na fasihi hutozwa asilimia 1.5 kila vinapoingia, kuzalishwa au kuundwa hapa nchini. Fedha hizo hukusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)” ameeleza Bi. Sinare.

Lengo kuu la kuanzishwa kwa tozo hiyo ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi wadau wa sanaa na uandishi nchini wakiwemo wasanii, waandishi na wabunifu ambao kwa muda mrefu kazi zao zimekuwa zikitumika katika mazingira mbali mbali ya kijamii kama vile kuhifadhi, kubebea na kusambaza kazi sanaa na uandishi na kuwanufaisha wadau wengine pamoja na watu binafsi bila ya wenye kazi kupata haki zao.

“Kupitia chanzo hiki, COSOTA imekusanya jumla ya Tshs. 1,428,105,241.44 kuanzia Septemba, 2023 hadi Februari, 2025 ambapo Ofisi imefanikiwa kupokea fedha za tozo ya hakimiliki za mwaka wa fedha 2023/2024 kutoka Wizara ya Fedha kiasi cha Tshs. 847,985,594.26.” ameongeza Bi. Sinare.

Aidha, amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, usajili wa kazi zinazolindwa na Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki umeongezeka kwa asilimia 70 ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kuanzia mwaka 2021 mpaka Februari 2025, COSOTA imesajili kazi za sanaa na uandishi 11,519 na wabunifu 3,436.

Mwaka 2021 - 2025, COSOTA imefanikiwa kufanya migao miwili kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alipolihutubia bunge mwaka 2021 ambapo alisisitiza katika kipindi cha uongozi wake Serikali itahakikisha wabunifu wote wananufaika zaidi na kazi zao.

Mgao wa kwanza unaotokana na matumizi ya kazi katika maeneo ya biashara pamoja na makusanyo ya maonesho kwa umma na vyombo vya utangazaji ulifanyika mwaka 2022 na ulikuwa ni mgao wa ishirini na tatu ulikuwa wa kiasi cha shilingi 312,290,259,000 ambapo Wasanii wa Muziki 1,123 walinufaika, na ulitokana na matumizi ya kazi 5,924 za Muziki ambazo zilitumika katika vituo 11 vya Redio, ikiwemo redio za ngazi ya Kitaifa, Mkoa, Wilaya, Kijamii na za Kidini.

Mgao wa pili wa mirabaha  wa matumizi ulikuwa mwaka 2023 na ulikuwa ni mgao wa ishirini na nne kwa Wasanii wa Muziki  na COSOTA iligawa kiasi cha shilingi 396,947,743.20  ambapo wasanii wa muziki 8,165 walinufaika, kupitia kazi 61,490 za muziki, kutoka vituko vya redio 14,vya kitaifa, mikoa, wilaya, jamii na za kidini.

COSOTA imeahidi kuendelea kutekeleza majukumu yake ya usimamizi wa hakimiliki katika kazi za sanaa ikiwa ni kuimarisha dhana ya kuhakikisha wasanii na waandishi wananufaika zaidi na kazi zao.

Pamoja na hayo ongezeko la usajili wa kazi COSOTA imetokana na zoezi la utoaji wa elimu na mafunzo mbalimbali ya hakimiliki na usajili kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, semina lakini pia kushiriki matukio mbalimbali ya wadau ambapo COSOTA ilipata fursa ya kuelimisha wadau kuhusiana na hakimiliki na uhamasishaji wa usajili wa kazi za hakimiliki.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi