Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imenunua jumla ya vichwa 17 vya treni ya umeme, vyenye mwendokasi wa 160km/h.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Bw. Masanja Kadogosa amesema hayo leo Machi 22, 2025 katika Ofisi za Idara ya Habari-MAELEZO wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa TRC katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Serikali kupitia TRC ilisaini mkataba na kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini tarehe 14 Julai, 2021 kwa ajili ya ununuzi wa vichwa vya treni ya umeme 17 vyenye mwendokasi wa 160km/h, hadi kufikia Desemba, 2024 vichwa vyote vya treni ya umeme 17 vimewasili na kuanza kutoa huduma,” amesema Bw. Kadogosa.
Vilevile, TRC ilisaini mkataba na kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini tarehe 14 Julai, 2021 kwa ajili ya ununuzi wa seti 10 za treni za abiria za umeme (Electric Multiple Unit – EMU), ambazo tayari seti zote 10 zimewasili nchini na kufanyiwa majaribio.
Aidha, tarehe 8 Februari, 2022 TRC ilisaini mkataba na Kampuni ya China Railway Rolling Stock Corporation (CRRC) - International Corporation Limited ya China kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa ya mizigo 1,430 yatakayotumika kutoa huduma pindi ujenzi utakapokamilika. Kati ya mabehewa hayo, mabehewa 264 (200 container carrier na 64 Covered wagon) yaliwasili nchini tarehe 11 Desemba, 2024 na yanaendelea na majaribio.
“Serikali kupitia TRC ilisaini mkataba na Kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Limited - SSRST ya Korea Kusini kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa 59 ya abiria. Vilevile, ilisaini mkataba na Kampuni ya Lueckermeier ya Ujerumani kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa 30 ya abiria. Hadi kufikia Desemba, 2024 mabehewa 71 ya abiria yamepokelewa na mabehewa 18 ya abiria yaliyosalia yanatarajiwa kuwasili kwa nyakati tofauti mwaka huu 2025,” amesema Bw. Kadogosa.
Pia, tarehe 7 Novemba, 2022 TRC ilisaini mkataba na Kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Limited - SSRST ya Korea Kusini kwa ajili ya ununuzi wa vifaa, mashine na mitambo ya matengenezo ya njia. Hadi kufikia mwezi Desemba 2024 kazi ya usanifu na uundaji umefikia asilimia 60.
Sambamba na utekezaji wa miradi ya SGR, shirika limeendelea na utekelezaji ya miradi kwa ajili ya kuboresha reli ya kati ya MGR, ikiwemo ukarabati wa Reli ya Kati ya Dar es Salaam – Isaka (Awamu ya Kwanza), ukarabati wa njia ya reli hadi uwezo wa ratili 80
Miradi mingine ni ukarabati wa Reli ya Kaliua – Mpanda (210KM), ambapo kazi zinazofanyika ni pamoja na kuboresha njia kwa kutumia reli za ratili 80, pamoja na ukarabati wa madaraja.
Vile vile TRC inatekeleza ujenzi wa Daraja na Mabadiliko ya Njia Kati ya Godegode na Gulwe, ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 175 katika km 349+450 (Kati ya Stesheni ya Godegode na Gulwe) na urekebishaji wa njia kwa urefu wa km 6.2.