Benki ya Maendeleo TIB imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 408.3 katika miradi ya maendeleo kwenye sekta zinazogusa wananchi.
Akieleza mafanikio katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Machi 20, 2025, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bi. Lilian Mbassy amesema, kati ya uwekezaji uliofanyika ni kwenye mifuko 9 yenye thamani ya shilingi bilioni 222.
"Kupitia uwekezaji huu, zaidi ya ajira mpya 12,547 zimezalishwa kutokana na benki kufadhili miradi ya maendeleo ya muda wa kati na mrefu nchini", alisisitiza Bi. Mbassy
Akifafanua amesema, TIB itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi ili kufikia azma ya Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha mazingira ya uwekezaji wa moja kwa moja wa ndani na nje kwa maendeleo ya wananchi na ustawi wa kiuchumi wa Tanzania.
Mwelekeo wa TIB ni kuwekeza kwenye miradi ya ujenzi wa Makazi, Elimu, Utalii, Afya na Upanuzi wa Bandari Kavu.