Na Jonas Kamaleki
Zaidi ya vijana 2340 wenye umri wa miaka kati ya 16 na 37 wameamua kujiondoa kwenye mtandao wa mazoezi ya kigaidi na kujisalimisha ili kuishi maisha ya amani na maadili mema baada ya kukutana na ushauri wa Jopo laViongozi wa Kamati ya kitaifa ya Maadili ,Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini zote nchini.
Hayo yalisemwa leo (jana) na Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya Maadili ,Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini zote nchini, Askofu William Mwamalanga katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Askofu Mwamalanga, vijana hao kutoka vijiji mbalimbali vya huko Ikwiriri na Kibiti wamesema walitumbukia kwenye uhalifu huo mwaka 2011 ambapo baadhi ya viongozi wa dini moja kutoka jijini Dar e Salaam walipita kuhamasisha vijana kujiunga nao na kuachana na dini ya kiislamu kisha kujiunga na mafundisho yanayotofautina na uislamu ya kuua viongozi wote na wananchi ambao walikataa kuliunga mkono.
Imeelezwa kuwa asili ya kundi hilo ni mafundisho yanayopinga uislamu na limejikita kwenye wilaya za Kinondoni, Temeke, Mbagala na Mikoa ya Tanga, Kagera, Morogoro, Dodoma, Lindi, Mtwara, Pemba, Tabora na Pwani. Kundi hilo limekuwa likifundisha vijana kujiunga na ugaidi kwa muda mrefu katika maeneo ya Songea, Tunduru, Ikwiriri, Kibiti, Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma bila hatua zozote za kuzuia, aliongeza Askofu Mwamalanga.
“Vijana hao wamekiri kuachana na mtandao wa kundi hilo huku wakiwaomba viongozi wa dini ya kiislamu nchini kukemea mafundisho ya kareti na ugadi kwenye baadhi ya misikiti”, alisema Askofu Mwamalanga.
Aidha, Kiongozi huyo wa Dini alisema kuwa kundi hilo lilikuwa linawahimiza wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wakiume na wasichana kuacha masomo na kuolewa na wavulana kujiunga na kundi hilo na wengine kupelekwa nje ya nchi kujiunga na shule za ugaidi hii ndiyo siri ya vijana wengi kwenye mikoa hii kujiunga na mtandao huo na wengi kutoendelea na masomo.
Askofu Mwamalanga aliongeza kuwa vijana hao wamempongeza Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kwa uthubutu wake na waledi wa wa kuifanya Rufiji na Ikwiriri kuwa eneo la amani hii itasaidia hata wanafunzi kusoma kwa amani na hasa wasichana wengi ambao wamepewa uja uzito na kutelekezwa na wengine wapo jijini Dar es Salaam ambako wanaishi maisha duni kwa hofu ya kuuliwa .
“Ninalaani vikali mafundisho ya uhalifu kufundishwa kwenye nyumba za ibada na nawahimiza vijana hao kuwa askari wa siri wa kufichua waharifu wote na kuwataka wale waliojificha misituni kujisalimisha kama wenzao”,alisisitiza Askofu Mwamalanga
Aidha, Askofu huyo amewataka watendaji wa Serikali ngazi ya Halmashauri wakiwemo wakuu wa wilaya kuwapatia vijana ardhi na kuwakamata mara moja watu wanaoeneza elimu ya chuki kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni Twahuti jina linalomaanisha kuwa Serikali hii siyo ya dola la kiislamu.
Kwa upande wao baadhi ya wazee 140 walioshiriki kwenye maombi na dua maalumu ya kuombea kukomesha mauaji hayo wamekiri kuwa mauaji hayo hayana uhusiano wowote na dini ya kiislamu wala siasa bali ni uharifu kama uharifu mwingine .
Hivi karibuni Serikali imeimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya Ikwiriri na Rufiji pia Kibiti ili kudhibiti mauaji yaliyokuwa yakijitokeza katika maeneo hayo. Kwa sasa hali imetulia na amani inaanza kurejea.