Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Awaasa Watumishi Wanaofanyakazi Viwandani
Jul 30, 2017
Na Msemaji Mkuu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasihi Watanzania wanaofanya kazi katika viwanda mbalimbali nchini kufanya kazi kwa bidii na kuwa waaminifu.

Amesema Tanzania imedhamiria kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda hivyo ni vema watakaopata fursa ya ajira katika viwanda hivyo kuwa waadilifu.

Ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 30, 2017) wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha gesi cha Ikama kilichoko wilayani Rungwe.

Waziri Mkuu amesema wakati Serikali ikiendelea kuwakaribisha wawekezaji nchini, wananchi walioajiriwa kwenye maeneo hayo wawe waaminifu.

“Mnatakiwa muwe waaminifu, msibebe kitu chochote ndani ya kiwanda bila ya ridhaa ya wamiliki kwa kuwa mtaonyesha taswira mbaya kwa wawekezaji.”

Amesema uaminifu wao ndio utawezesha Watanzania wengi kupata ajira kwenye viwanda hivyo ambavyo vimejengwa  katika maeneo yao.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na kampuni ya TOL Gases, Mhandisi  Harold Temu alisema kiwanda kinauwezo wa kuzalisha tani 46 kwa siku.

Alisema gesi inayozalishwa kiwandani hapo ni ya Carbon Dioxide ambayo inauzwa nchini na nchi jirani za Zambia, Malawi, Zimbabwe na Congo.

Mhandisi Temu alisema wateja wakubwa wa gesi hiyo ni viwanda vya kutengenezea soda, bia na pia hutumika katika kuhifadhia chakula na kwenye vifaa vya kuzimia moto.

Mapema Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kuchakata majani ya chai cha Katumba, ambapo alisema Serikali inaimarisha Ushirika wa zao hili ili wakulima waweze kupata tija.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, JULAI 30, 2017

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi