Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Mwenyeji Mkutano wa Majaji Mahakimu wa Jumuiya ya Madola
Sep 21, 2017
Na Msemaji Mkuu

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mkutano wa kumi wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola utakaofanyika kuanzia Septemba 25 - 27  mwaka huu jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Wambali.

Na. Paschal Dotto- MAELEZO.

Kwa mara ya kwanza Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa 10 wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Jumuiya ya Madola unaotarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 25 – 27 mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu.

Akizungumuza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam Jaji  Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa huu utakuwa ni mkutano wa kihistoria kwa Tanzania kwani ni mara ya kwanza kufanyika tangu kuanzishwa kwa chama hicho.

Alieleza kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo utakaohudhuriwa na wajumbe Zaidi ya 354, unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Makamu wa Rais, Mhesimiwa Samia Suluhu Hassan.

 “Mkutano huu mkubwa katika historia ya nchi yetu ni muhimu sana hasa katika sekta yetu ya utalii kwani tutapata kutangaza vivutio vyetu vya utalii, tunawaomba wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuwepo ili kutangazo sekta ya utalii”, alisema Prof. Juma.

Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Wambali akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mkutano wa kumi wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola utakaofanyika kuanzia Septemba 25 - 27  mwaka huu jijini Dar es Salaam. kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma.

Akieleza umuhimu wa mkutano huo Prof. Juma alisema kuwa mkutano huu utawajengea uzoefu na uelewa mkubwa Mahakimu na Majaji wa mahakama ya Tanzania kwani wapata kujua kuhusiana na masuala ya uhuru wa mahakama, masuala mikataba ya kimataifa, maendeleo ya kisheria na upatikanaji wa huduma ya haki.

Aidha Prof. Juma alisema kuwa kati ya washiriki kutoka Tanzania watapata uzoefu wa sheria katika maeneo mageni kama sheria mpya za kushughulika na magaidi duniani na mitandao ambapo uvunjwaji wa sheria umekuwa mkubwa sana.

“Kwetu Tanzania mkutano huu ni muhimu sana kwa sababu majaji na mahakimu wetu wapatao 50 ambao watahudhuria watapata fursa ya kujengewa uwezo na kubadilishana uzoefu na wale wanaohudhuria hasa kwa maeneo ambayo ni mapya kwa mfano jinai za kigaidi, makosa ya kimutandao ni maeneo ambayo yahitaji uzoefu wa kutosha”, alieleza.

Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma (hayupo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu mkutano wa kumi wa Chama cha Majaji na Mahakimu wa Jumuiya ya Madola utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 25 - 27 Septemba mwaka huu.

Aidha Prof. Juma alisema kuwa mada mbalimabli zitatolewa katika mkutano huo kama kukabiliana na vizuizi katika upatikanaji wa haki, rushwa, utovu wa maadili pamoja na uendeshwaji wa kesi katika maeneo mapya kama ughaidi na makosa ya kimutandao  huku Tanzania wakipewa kuwasilisha  mada katika maeneo ya ujangili na uboreshaji wa upatikanaji wa haki mahakamani.

Tanzania ni mwanachama halali wa Chama Majaji na Mahakimu kutoka nchi za Jumuiya ya Madola tangu mwaka 1970 huku mkutano huo ukifanyika kwa mara ya kwanza kwa Tanzania.Mara ya mwisho mkutano huo ulifanyika Guyana, Amerika ya kusini ambapo mahakama ya Tanzania ilituma wawakilishi wake.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi