Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TADB Yatoa Mikopo kwa Wakulima 2,252
Sep 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.

Jumla ya Wakulima 2,252 wamenufaika na mikopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambapo jumla ya shilingi Bilioni 7.46 zimetolewa hadi kufikia Juni, 2017.

Hayo yameelezwa leo Bungeni, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbeya Vijijini Oran Manase Njeza juu ya mikopo iliyotolewa na Benki hiyo mpaka sasa.

“Mpaka sasa TADB imetoa mikopo katika mikoa ya Tanga, Morogoro na Iringa, aidha wakulima wanaonufaka na mikopo hiyo ni wale walio katika vikundi au vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS),” alifafanua Ole Nasha.

Ameendelea kwa kusema kuwa, mpaka kufikia Juni, 2017 TADB imefikisha mtaji wa shilingi bilioni 65.6 ambapo umepanda kutoka shilingi 65.3 kama ulivyokuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2017.

Aidha, kutokana na udhamini wa Serikali, Benki hiyo imepata mkopo wa bei nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wa kiasi cha Shilingi Bilioni 209.5 fedha ambazo zinatolewa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza zimetolewa shilingi Bilioni 104.6

TADB inalenga kufungua Ofisi za Kanda nchi nzima ili kurahisisha na kupunguza gharama za upatikanaji wa mikopo. Aidha wakulima walio katika vikundi au vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) ndio watakao nufaika na mikopo ya TADB kuanzia msimu ujao wa kilimo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi