Na: Immaculate Makilika
Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT), linatarajia kuanzisha kiwanda cha kusindika minofu ya nyama ya ng’ombe na samaki na kampuni ya kusambaza nyama kwa nia ya kuunga mkono azma ya Serikali ya awamu ya tano ya kuelekea katika uchumi wa viwanda.
Akizungumza katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Idara ya Habari, (MAELEZO) na kurushwa na kituo cha televisheni cha TBC1, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMA JKT Brigedia Jenerali Charo Yateri alisema kuwa shirika hilo pia limedhamiria kutoa mafunzo kwa vijana kupitia miradi mbalimbali ambayo ipo chini ya shirika hilo.
“SUMA JKT imeendelea kujiimarisha kupitia miradi yake ya kilimo, huduma za ulinzi, uvuvi pamoja na ufugaji, ambapo ina viwanda vya kusindika na kuchakata mazao, na asali ambapo kupitia miradi na viwanda hivyo imetoa ajira 4,500 kwa vijana nchini” alisema Brigedia Jenerali Yateri.
Alitaja viwanda hivyo kuwa ni viwanda vya kusindika asali mkoani Tabora, viwanda vya kusindika na kuchakata nafaka vilivyopo Mlale mkoani Ruvuma na Mafinga mkoani Njombe.
Mbali na hayo, Brigedia Jenerali Yateri alisema kuwa SUMA JKT ina miradi mbalimbali ikiwemo ya kujenga majengo ya Halmashauri, barabara kwa gharama nafuu, ubora na uharaka Nna wana mpango wa kujenga nyumba za wanajeshi kwa ajili ya kuwakopesha.
“ Tunaendelea kufanya mazungumzo na benk ya Azania ili tujenge nyumba za wanajeshi ambapo wataweza kupewa mikopo ya kununua nyumba hizo, na baadae tutaanza kujenga nyumba kwa wananchi” alisema Brigedia Jenerali Yateri.
Alitaja huduma nyingine zinazofanywa na shirika hilo kuwa ni pamoja na kuuza zana bora za kilimo kama matrekta, pampu za maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, kufundisha jamii kilimo, uzalishaji wa mbegu bora za nafaka na mradi wa mabwawa ya kufuga samaki katika vizimba vya ziwa Victoria
Aidha, Brigedia Jenerali Yateri alisema SUMA JKT inajivunia miradi hiyo sambamba na kuwa na kilimo cha mazao ya biashara kama vile kahawa mkoani Mbeya na mchikichi mkoani Kigoma, sambasamba na uwezo wa kujitegemea kwa asilimia 55, huku ikipata ruzuku ya serikali asilimia 45 tu.
Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT), lilianzishwa mwaka 1982, kwa tamko la Rais chini ya sheria ya uanzishaji wa mashirika ya ummakwa lengo la kuisaidia serikali kupunguza gharama za kuendesha mafunzo kwa vijana wanaopatiwa ujuzi wa aina mbalimbali ili kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Taifa kwa ujumla.