Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

SERIKALI YATOA FEDHA 100% YA MANUNUZI YA DAWA NCHINI
May 16, 2017

Na. Immaculate Makilika.

  Serikali imetoa  asilimia mia moja ya fedha za bajeti ya dawa kwa mwaka  2016/2017  kwa ajili ya manunuzi ya dawa ikiwa ni moja ya mikakati ya kuboresha sekta ya afya nchini.   Akizungumza katika mahojiano ya kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari – MAELEZO na kurushwa  na kituo cha televisheni cha TBC, Mkurugenzi  Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa,  Laurean Bwanakunu alisema kuwa Serikali inawahakikishia  wananchi kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 zipo  fedha za kutosha ili kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya.   “Ikiwa ni  asilimia  81 ya upatikanaji wa dawa  pamoja na vifaa tiba katika maeneo ya mjini na vijijini, ambapo Bohari Kuu ya Dawa inahudumia vituo 5642 nchini kote” alisema Bwanakunu.   Pia, Bwanakunu alibainisha kuwa  hivi sasa kumekuwepo na upatikanaji wa dawa muhimu 110 kati ya 135   katika vituo  mbalimbali  vinavyotoa huduma za huduma  za afya.   Katika kuboresha huduma za usambazaji wa dawa nchini , Bohari Kuu ya Dawa imefanikiwa kufungua maduka ya dawa 7 katika mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Geita, Mbeya  na Lindi, ambapo  imeanza kusafirisha dawa kwa kutumia  ndege na treni ili kufikisha dawa kwa wakati katika vituo mbalimbali vya afya nchini.   Aidha,  Mikoa na Halmashauri  zimetakiwa  kuwasilisha  maombi yao ya  dawa kwa wakati ili kutatua changamoto ya upungufu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya.  
 

Mipangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi