Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 21, 2023 amezindua Mitambo 5 ya Uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo pamoja na vifaa kazi vingine vya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) vyenye jumla ya thamani ya shilingi 9,178,559,128.
Uzinduzi huo umefanyika katika Kituo cha Mkutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma ambapo umeenda sambamba na kukabidhi vifaa hivyo kwa wachimbaji wadogo wakiwemo Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA) na Chama cha Wachimbaji Wanawake Tanzania (TAWOMA) ambapo vinajumuisha mitambo mitano ya uchorongaji yenye thamani ya shilingi bilioni 2.22.
Vifaa vingine ni pamoja na Lori tatu za kubeba vifusi vya madini (Dump trucks) zenye thamani ya shilingi milioni 544, Lori moja la kubeba mitambo (Lowbed) lenye thamani ya shilingi milioni 274, mtambo mmoja wa kusaga makaa ya mawe (Coal Crusher) wenye thamani ya zhilingi bilioni 1.58.
Pia amekabidhi mtambo mmoja wa kusaga miamba kwa ajili ya kokoto (stone/aggregate crusher) wenye thamani ya shilingi bilioni 1.137, mtambo mmoja wa kufua upepo yaani Air compressor wenye thamani ya Shilingi milioni 424, Lori moja la kubebea maji (water bowser) lenye thamani ya shilingi milioni 210.
Vilevile amekabidhi mitambo miwili ya uzalishaji wa mkaa mbadala (Rafiki Briquettes) wenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa saa yenye thamani ya shilingi bilioni 2.396, magari mawili (2 hardtop) kwa ajili ya shughuli za uzalishaji madini migodini yenye thamani ya shilingi milioni 317 na Jaw Crusher 10, Metal Detector (20) na Injini ya Dizeli aina ya 24HP moja vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 72.5.