[caption id="attachment_6849" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Januari Makamba (MB) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa uamuzi wa kutengua uteuzi wa wajumbe saba wa Bodi ya Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) na uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Profesa Faustine Kamuzola. (Picha na: Frank Shija)[/caption]
Na: Frank Mvungi
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Januari Makamba (Mb) ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ili kuongeza tija na kutekeleza kwa vitendo dhana ya Ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Kwa kuzingatia mamlaka aliyonayo Waziri chini ya Sheria ya Mazingira kifungu cha 19 (2) anaweza kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Baraza hilo na wajumbe wake.
[caption id="attachment_6850" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Januari Makamba (MB) akifafanua jambo mbele yanwaandishi wa habari (hawapo pichani) akitangaza uamuzi wa kutengua uteuzi wa wajumbe saba wa Bodi ya Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) pamoja na uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Profesa Faustine Kamuzola na kulia ni Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Richard Muyungi.[/caption]Akizungumza na vyombo vya Habari leo Jijini Dar es Salaam Waziri Makamba amesema kuwa lengo la mabadiliko hayo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na usimamizi na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira na uharakishaji wa miradi ya maendeleo na uwekezaji hasa ujenzi wa viwanda kama azma ya Mheshimiwa Rais John Magufuli inavyoelekeza.
Kufuatia mabadiliko hayo Waziri Makamba amemteua Dkt. Elikana Kalumanga ambaye ni Mhadhiri katika Taasisi ya Usimamizi na Tathmini ya Rasilimali Asili,Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC hadi Rais atakapoteua Mkurugenzi Mkuu.
“Utendaji wa NEMC umekuwa ukilegalega sana na umekuwa hauridhishi na kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuhusu ucheleweshaji na urasimu usiokuwa wa lazima katika mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira (EIA)” Alisisitiza Mhe. Makamba
Aliongeza kuwa ametengua uteuzi wa wajumbe wote saba wa Bodi ya NEMC ili baadaye ateue wajumbe wapya ambao wataendana na kasi na ari ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuelekea uchumi wa Viwanda, ambapo Mwenyekiti wa Bodi ambaye mamlaka yake ya uteuzi ni Mheshimiwa Rais,ataendelea kuwepo hadi Mheshimiwa Rais atakapoteua mwingine.
[caption id="attachment_6853" align="aligncenter" width="750"] Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa kazini wakati wa mkutano wao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Januari Makamba (MB) alipokuwa akitangaza uamuzi wa kusitisha uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) na wajumbe saba wa Bodi ya baraza hilo leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na: Frank Shija)[/caption]Akifafanua Makamba amesema kuwa changamoto nyingine zilizobainika ni kuwaelekeza wawekezaji kwa makampuni ya kufanya Tathmini ya athari za mazingira ambayo yanamilikiwa au yenye ubia na watumishi wa NEMC, bila kujali mgongano wa kimaslahi jambo ambalo haliruhusiwi katika utumishi wa umma.
Jambo jingine ni kuwarundikia maandiko ya miradi ya tathmini ya athari kwa mazingira (EIA) watumishi wachache wakati wengine hawana kazi ili waelekeze miradi hiyo katika makampuni ambayo baadaye huwapatia malipo yasiyo halali.
Hatua nyingine zilizochukuliwa na Waziri Makamba ni pamoja na kuiagiza NEMC kufuta watu binfsi na Makampuni yote ya ushauri wa EIA (Consultants) ambayo hayana sifa au yameshindwa kutekeleza kazi zao vizuri na watangaze kwenye magazeti orodha ya watu na makampuni yanayoruhusiwa kufanya kazi kama washauri elekezi.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC ni muhimu katika kuhakikisha ustawi wa mazingira na mustakabili wa maendeleo endelevu ya nchi tunapoelekea kuwa Taifa la uchumi wa viwanda lazima usimamizi wa mazingira uwe thabiti.