[caption id="attachment_3680" align="aligncenter" width="750"] Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia kwenye Tamasha la Uelimishaji na Upimaji Afya na Kinga dhidi ya Magonjwa yasiyoambukiza kwa watoto na vijana kwenye uwanja wa michezo wa shule ya msingi Kinyerezi.[/caption]
Na Jacquiline Mrisho.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuwafichua watu wanaonyanyasa na kudhalilisha watoto kijinsia ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Mhe. Samia ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akihitimisha kampeni ya kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika viwanja vya Shule ya msingi Kinyerezi vilivyopo jijini humo.
Vile vile amesema, watu wanaofanya vitendo vya udhalilishaji wa watoto wapo miongoni mwa jamii hivyo ni jukumu la Serikali, walezi na wazazi kuwafichua watenda maovu hao ili kukomesha vitendo hivyo na kuwafanya watoto waishi kwa amani nchini.
[caption id="attachment_3679" align="alignnone" width="745"] Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiteta jambo na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamis Kigwangalla wakati Tamasha la Uelimishaji na Upimaji Afya na Kinga dhidi ya Magonjwa yasiyoambukiza kwa watoto na vijana kwenye uwanja wa michezo wa shule ya msingi Kinyerezi. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)[/caption]”Katika kukabiliana na hali hiyo, nimeviagiza vyombo vya dola kutofumbia macho vitendo hivyo pindi wanapopata taarifa za matukio ya udhalilishaji wa watoto na badala yake wachukue hatua za haraka za kuwakamata na kuwachukulia hatua stahiki watu wanaofanya vitendo hivyo vibaya,” alisema Mhe. Samia.
Makamu wa Rais ameongeza kuwa kufanya hivyo kutawasaidia watoto kuwa salama katika mazingira ya nyumbani hata wakiwa mashuleni kwani watu wabaya wanaofanya vitendo hivyo watawajibishwa kulingana na matendo maovu wanayoyafanya watoto.
Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kote nchini kuwapatia taarifa Walimu wao na Polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanyika Juni 16 kila mwaka tangu ilipotangazwa rasmi na jumuiya ya Umoja wa Afrika mnamo mwaka 1991.