Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Gereza la Kwitanga Lipatiwe Kiwanda cha Kisasa - Majaliwa
Feb 18, 2019
Na Msemaji Mkuu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara ihakikishe gereza la Kwitanga mkoani Kigoma linapata kiwanda bora na cha kisasa cha kukamulia mafuta ya mawese kitakachoonesha dhamira ya Serikali ya kufufua zao la michikichi nchini.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na jitihada zilizofanywa na Jeshi la Magereza katika kuboresha shamba lake la michikichi pamoja na mabadiliko waliyoyafanya kwenye kiwanda chao cha kuzalisha mafuta.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Februari 17) wakati alipotembelea Gereza la Kwitanga kwa ajili ya kukagua shamba la michikichi na kuzindua trekta na kufungua sero moja iliyojengwa gerezani hapo.

Amesema amefurahishwa baada ya kukuta mashine mpya ya kukamulia mafuta ya mawese inafungwa kwenye kiwanda cha gereza hilo ambayo itakuwa inatumia mota tofauti za zamani wapolikuwa wanatumia mashine ya kusukumwa na mikono.

Kadhalika Waziri Mkuu ameliagiza Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) waimarishe teknolojia ya kukamua mafuta kwenye kiwanda hicho ili kiweze kuzalisha kwa tija.

Katika kuhakikisha gereza hilo linakuwa la mfano kwenye kilimo cha zao la michikichi, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inunue gari lenye winchi litakalorahisisha uvunaji wa chikichi.

Waziri Mkuu amesema njia inayotumiwa kwa sasa ya kupanda juu ya mchikichi wakati wa mavuno si salama kwa mvunaji, hivyo ni vema wakatumia magari hayo yenye winchi kwa ajili ya kurahisisha shughuli ya uvunaji.

Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kigoma, Leonard Burushi amesema wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa mafuta kutoka pipa 63.4 kwa mwaka 2016/2017 na kufikia pipa 97 kwa mwaka 2018/2019 na zoezi la uvunaji bado linaendelea.

Amesema mafanikio hayo yametokana na maagizo yalitolewa na Waziri Mkuu alipotembelea gereza hilo Julai, 2018, ambapo pamoja na mambo mengine aliwaagiza waboreshe eneo la kukamulia mafuta ili waongeze uzalishaji.

Kiongozi huyo wa Magereza mkoa wa Kigoma amesema eneo la ekari 20 limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kukamua mafuta ya mawese, maghala ya kutunzia mafuta machafu na upanuzi wa kiwanda baadae.

Amesema maelekezo mengine yaliyotolewa na Waziri Mkuu ni pamoja na Magereza ya Kwitanga na Ilagala yaongeze eneo la mashamba yake kwa ajili ya kupanda michikichi mipya ambalo limetekelezwa.

Amesema tayari gereza la Ilagala limeandaa jumla ya ekari 150 zenye uwezo wa kupandwa michikichi aina ya tanera 8,550 na Kwitanga ekari 400 ambazo zitapandwa miche 22,800 ya michikichi aina ya tanera.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMAPILI, FEBRUARI 17, 2019.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi