Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Chuo Kikuu Kipya Kuanzishwa Ili Kuunga Mkono Juhudi za JPM Kuzalisha Watoa Ajira.
Jul 17, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Thobias Robert

Taasisi ya Kiislam ya The Registered Trustees of Masjid Ridhwaa (RTMR), imedhamiria kuanzisha Chuo Kikuu mahsusi kwa ajili ya kuwaandaa vijana wa Kitanzania kujiajiri tofauti na ilivyo sasa kwa baadhi ya vyuo kuandaa wahitimu wanaotegemea kuajiriwa.

Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa Taasisi  hiyo, Alhaj Suleiman Seif Nassor, alisema lengo na dhumuni la taasisi yake ni kuanzisha Chuo Kikuu kitakachoendana na zama hizi za kidijitali za kuzalisha wataalam watakaoweza kujiajiri wenyewe kwa kutumia teknolojia zilizopo.

“Chuo Kikuu tunachotarajia kuanzisha kitatoa wahitimu ambao wao wenyewe watakuwa wenye kujiajiri na pia kutoa ajira tangu siku ya kwanza ya kuhitimu shahada zao,” alisema Mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa mifumo ya utoaji wa Elimu iliyopo katika Vyuo Vikuu  vingi hapa nchini, inamjenga mwanafunzi kuwa tegemezi wa Serikali na mashirika binafsi ili yamuajiri lakini wao kama Taasisi yenye lengo la kuendana na sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda wana mpango wa kubadilisha mfumo na mtazamo huo.  

“Ili kuendana na sera za awamu hii, taasisi imetafakari kwa kina pamoja na kufanya tafiti mbalimbali na    kubaini kuwa ni lazima tubadili muundo wa utoaji shahada uliopo sasa wa kuandaa watafuta ajira,na badala yake tuandae wataalamu watakaojiajiri na kuajiri wenzao.

Shahada zinazotarajiwa kuanzishwa ili kuendana na halihalisi ya soko la sasa, pamoja na mabadiliko ya kisayansi na teknolojia nipamoja na BSc. Enterpreneur management, BSc. Agricultural Bussiness, Freelance Photo Journalism pamoja na Corporate communication.

Aidha kwa upande wa miundombinu Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa tayari walishaanza kujenga jengo la Chuo hicho lenye ghorofa tano  na amewaomba watanzania wenye kiu ya maendeleo kujitoa kwa hali na mali kuchangia ujenzi, ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwakomboa watanzania katika lindi la umaskini.

Wakati huohuo Mwenyekiti huyo wa taasisi ya RTMR amepongeza juhudi zinazofanywa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kupambana na ubadhirifu wa mali za uuma pamoja na kuleta uwazi na uwajibikaji katika utumishi wa umma.

“Mh.Rais ameonyesha dhamira ya dhati kupambana na madawa ya kulevya ambayo yameathiri vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa, hivyo nasisitiza sisi kama viongozi wa dini na watanzania wote kwa ujumla tumuombee dua ili aweze kukamilisha ndoto yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi  yenye neema “ Alisema.

Miongoni mwa shughuli za kimaendeleo zinazofanywa na taasisi ya RTMR ni pamoja na Kujenga misikiti, Vituo vya Afya, Vituo vya Elimu, pamoja na miradi ya kujikwamua kiuchumi kwa kuzingatia misingi ya kiislam.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi