Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

RAS Tabora Awataka Ma-DED Kuwaondoa Wavamizi Maeneo ya Shule.
May 29, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent –RS Tabora

Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dkt. Thea Ntara amewaagiza Wakurugenzi wote wa Manispaa na Halmashauri mkoani humo kuhakikisha wanawaondoa haraka watu waliovamia maeneo ya Taasisi na Shule na kujenga makazi yao.

Dkt. Ntara alitoa agizo hilo jana mjini Tabora wakati wa kikao na watendaji mbalimbali wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Alisema kuwa haiwezekana hadi hivi sasa watu waendelee kuishi katika maeneo ya Shule na Wakurugenzi Watendaji wamekaa kimya bila kuchukua hatua yoyote.

Aidha, Dkt. Ntara alisema kuwa zoezi la kuwaondoa wavamizi hao ni vema likaenda sanjari ya ujenzi wa uzio unazunguka eneo la shule husika ili kuzuia watu ambao watakuwa wameondoka kwa hiari na wale watakalazimishwa kuondoka kuweza kurejea tena.

Aliongeza kuwa ujenzi wa uzio huo sio lazima uwe wa gharama kubwa kwani wanaweza kutumia mbinu ya kupanda miti kuzunguka eneo la taasisi  au shule husika kama ulinzi na kuonyesha miapaka ya  eneo husika.

Aidha ,Dkt. Ntara alisisitiza kuwa wakati ukarabati wa shule kongwe kama vile Shule ya Wavulana na Wasichana za Tabora na Milambo ukitarajia kuanza hivi karibuni ni vema Wakurugenzi wakahakikisha maeneo ya shule hizo na nyingine wavamizi wameondoka.

Aliongeza kuwa uvamizi huo umesababisha wanafunzi na wanavyuo kukosa hata maeneo ya kuendesha elimu ya michezo kwa ajili ya maandalizi ya wataalam wa baadaye wa sekta hiyo.

Dkt Ntara alisema kuwa kuanzia sasa Watendaji wapite katika kila  shule zilizovamiwa na kuweka alama za X katika nyumba zilizojengwa katika shule.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi