Mhadhiri wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela na Mratibu wa Uhusiano wa Kitaaluma na Viwanda katika Mifumo iliyopachikwa na Simu (EMoS), Dkt. Judith Leo amewataka wanafunzi wa shule ya msingi Nganana na Nambala kuweka juhudi katika masomo ya Sayansi na Hisabati kwa kuwa siyo magumu kama ambavyo wanafikiri bali juhudi binafsi na kupenda somo kunaweza kuwafanya wafaulu vyema.
Dkt. Judith ameyasema hayo Machi 21, 2024 alipotembelea shule hizo akiwa ameongozana na wanafunzi wa Shahada ya Umahiri (CEMoS) wa Kituo cha Ubora cha TEHAMA Afrika Mashariki (CENIT@EA) katika ziara ya uenezi na huduma kwa jamii katika shule hizo mbili zilizopo Arumeru jijini Arusha lengo likiwa ni kuhamasisha umuhimu wa kuweka mkazo katika masomo hayo.
Aidha, wanafunzi wa Shahada ya Umahiri katika Mifumo iliyopachikwa na Simu (EMoS) walitoa elimu kwa vitendo ya namna ya kutumia vifaa mbalimbali vya kisayansi ikiwemo kompyuta, vifaa vya maabara katika kutambua matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii ili kuwapatia ufumbuzi wa kutatua changamoto hizo.
Naye, Mwanafunzi wa Shahada ya Umahiri katika Mifumo Iliyopachikwa na Simu (EMoS), Seth Odwar kutoka nchini Kenya amewahimiza wanafunzi hao kuzingatia somo la Hisabati ambalo wengi huhisi halina manufaa katika kozi nyingine na kuongeza kuwa sayansi ni muhimu katika kutatua changamoto za jamii.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Jackline Mushi ameishukuru Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa kutoa hamasa kwa vitendo pamoja na kuwajengea uwezo katika matumizi ya vifaa vya kisayansi ikiwemo kompyuta.
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela inatekeleza majukumu yake katika misingi mitano (5D Business Modal) ambapo mojawapo ya msingi huo ni Uenezi na Huduma kwa Jamii (Outreach na Community Engagement).