Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paul Makonda amefanya mazungumzo na Balozi wa Qatar hapa nchini Mhe. Ahmed Abdulla Al-Dossari kuhusu ushirikiano wa nchi hizo katika uwekezaji kwenye maendeleo ya sekta ya michezo hapa nchini.

Mhe. Waziri Makonda amekutana na Balozi huyo Februari 16, 2026 jijini Dar es Salaam, ambapo alimueleza namna Tanzania inavyoendelea na maandalizi kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 akibainisha fursa za uwekezaji katika miundombinu ikiwemo malazi jijini Arusha, uboreshaji wa viwanja vya mpira wa miguu, pamoja na kukuza sekta ya utalii.

Alisisitiza umuhimu wa kunufaika na uzoefu wa Qatar uliopatikana wakati wa kuandaa Kombe la Dunia la FIFA 2022, tukio lililotambulika kimataifa kwa ubora wa miundombinu, usimamizi na mchango wake mkubwa katika uchumi na maendeleo ya sekta ya michezo nchini humo.

Vilevile alishukuru nchi hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika sekta za maendeleo, uwekezaji na diplomasia.
. 
Kwa upande wake Balozi Ahmed alisisitiza kuendeleza ushirikiano huo kupitia kubadilishana uzoefu, kuendeleza miradi ya pamoja itakayochochea maendeleo ya michezo, utamaduni, utalii uwekezaji pamoja na uchumi.