Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Ummy Azindua Mpango wa Kutoa Huduma za Upasuaji wa Kibingwa Bila Malipo Jijini Tanga
Nov 06, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Oscar Assenga, TANGA.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Tanzania bado ina uhaba mkubwa wa Madaktari Bingwa hivyo uwepo wa mpango wa kambi ya upasuaji wa huduma za kibingwa unahitajika sio kwa mkoa wa Tanga bali ni mikoa yote nchini.

Ummy ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tanga (CCM) aliyasema hayo wakati akizindua mpango wa kutoa huduma za upasuaji wa kibingwa bila malipo kwa wakazi wa Jiji la Tanga uliofanyika kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo.

Alisema hivyo uwepo wa mpango huo utawasaidia wana Tanga na watanzania kwa ujumla kupata matibabu, dawa, vifaa tiba bila gharamu yoyote.

Mpango huo ambao utasaidia kufanya upasuaji utafanywa na Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya Peleks Humanitarian Organization ya nchini Uingereza ambapo jumla ya wagonjwa 380 watafaidika kati yao wagonjwa zaidi ya 700 waliofanyiwa uchunguzi.

Kambi hiyo ya matibabu Bingwa ya upasuaji imewezeshwa na Taasisi ya Watumishi Health Check, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Tanga mjini ambapo kwa pamoja wamewaleta wataalamu hao wa upasuaji kutoka nchini Uingereza.

Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi wa Watumishi Afa Check, Dkt. Siraji Mtulia alisema kuwa upasuaji huo utafanyika kuanzia Novemba 5 hadi 11 mwaka huu na utagharimu milioni 876.

Naye kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Kallage alisema uwepo wa kambi hiyo ni jitihada za Waziri Ummy kwa sababu ni jukumu ambalo amepewa na Rais Samia Suluhu kuhakikisha afya za watanzania vinaimarika na kuboresha huduma.

Alisema hata ukiangalia ile kampeni ya Mama Samia yeye ndio anaiendeleza ameanza na Tanga kwa kushirikiana na Peleck anataendelea na mikoa mengine nchini.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Jonathan Budemu alisema kwamba kambi hiyo itaweza kuwasaidia wananchi na katika watu 700 walioonwa na madaktari walikuwa hawana uharaka ule na muendelezo wa kambi hii utawasaidia kuweza kuwaona.

Alisema katika kambi hiyo watakuwa na changamoto ya vitanda hivyo wale ambao watakosa maeneo ya kuwaweka wanaomba kuwaweka kwenye vituo vyengine baada ya upasuaji kama Ngamiani na Makorora na vya jirani ili wote waweze kupata huduma kwa wakati.

“Lakini pia wasikose huduma kwa sababu ya kukosa sehemu ya kulala kwa sababu vitanda ni vichache ukilinganisha na wagonjwa wenyewe, hivyo wakishafanyiwa wakikosa nafasi hapo watapelekwa kwenye maeneo mengine”, alisema Dkt. Budemu.

Uzinduzi wa matibabu ya upasuaji wa Kibingwa pia imehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Kallaghe, Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga, Abdurhaman Shilloo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jonathan Budemu na viongozi wa CCM.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi