Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Ndalichako Aagiza Sababu za Mkandarasi Kuongeza Muda wa Ujenzi Kiwanda cha Sukari Mkulazi Kuchunguzwa
Jul 21, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, ameiagiza Bodi ya Kiwanda Cha Sukari cha Mkulazi kuzifuatilia na kuzichambua sababu ambazo zimekuwa zikitolewa na Mkandarasi  anayejenga Kiwanda cha sukari Mkulazi kushindwa kukamilisha ujenzi wa Kiwanda hicho ndani ya muda.


Mhe. Ndalichako ameeleza mkandarasi huyo kila unapofika muda wa kukamilisha ujenzi hutoa sababu ya kuongezwa muda, wakati ujenzi wa  Kiwanda hicho ulitarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu, lakini Mkandarasi ameomba aongezewe muda hadi mwezi  Machi mwakani.


Akiongea  leo tarehe 21 Julai, 2022 wilayani Kilosa, wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi huo, amesisitiza  kuwa Bodi hiyo kabla ya kumuongezea muda ihakikishe imejiridhisha juu ya sababu anazotoa.


"Huyu Mkandarasi abanwe muda anaoomba upungue hadi mwezi Desemba mwaka huu, tunataka kiwanda hiki kianze kuzalisha ili malengo ya Serikali ya Uwekezaji huu kupitia Mfuko wa NSSF yaweze kutimia.
Mhe. Ndalichako ameongeza kuwa lengo la Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia ni kuongeza fursa za ajira na Uwekezaji kwa watanzania kupitia kiwanda hicho.


Katika hatua nyingine; Mhe. Ndalichako ameutembelea Mradi wa machinjio  ya Kisasa ya Nguru wilayani Mvomero, Morogoro  ambapo amepongeza kwa hatua iliyofikiwa kwa kuwa mradi huo ukianza kufanya kazi utawezesha Kiwanda  kuongeza fursa za Ajira, kuongeza thamani ya mazao ya mifugo hivyo watanzania watanufaika.


Amefafanua kuwa Mhe. Rais Samia amekuwa akihamasisha uwekezaji, hivyo Serikali kupitia PSSSF imefanya Uwekezaji katika kiwanda hicho kwa kuwa kiwanda hicho  kitaiwezesha Serikali kupata fedha za kigeni na kukusanya Kodi.


Wakiongea kwa nyakati tofauti , Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi, Dkt. Hilideltha Msita, amesema  Bodi ya Kampuni Hodhi ya Mkulazi wameyapokea maelekezo na watayatekeleza Kwa  kuupitia Mpango kazi wa Mkandarasi ili kuweza kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake ukamilike mwezi Desemba mwaka huu.


Naye, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Mfuko wa PSSSF, Fortunatus Magambo amesema kiwanda cha Nguru kitakapoanza kufanya kazi kitakuwa kikichinja ngo'mbe 100 kwa siku na mbuzi 1000 kwa siku, Ajira za muda mrefu 350, Ajira 2000 zitakazotokana na  mnyororo wa thamani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi