Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watendaji wa Serikali wanaosimamia urejeshaji wa hali katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua mkoani Lindi wahakikishe wanarejesha kwa haraka huduma za usafirishaji.
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Machi 07, 2024) kwenye kikao kilichofanyika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam ili kupokea taarifa ya athari za mvua katika mkoa huo. Kikao hicho kiliwahusisha Mawaziri, Makatibu Wakuu na wataalam wengine wa Serikali
Aidha amesema kuwa, kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya barabara na baadhi ya maeneo ya Chibutuka na Nangano kutoweza kufikika kabisa, timu hiyo ya wataalam ihakikishe maeneo hayo yanapatiwa msaada wa haraka wa chakula.
“Malori ya Jeshi yatumike kufikisha vyakula vya msaada wa maafa hadi maeneo ya karibu kwa ajili ya kuwezesha ubebaji wa vyakula hivyo hadi maeneo yenye uhitaji kwa kutumia Helikopta”.
Amesema kutokana na Wilaya ya Liwale kutofikika kwa barabara zilizokuwa zikitumika awali, wataalam waweke jitihada za kuifungua barabara ya Nangurukuru - Liwale pia waone namna ya kuwezesha barabara ya Ruangwa- Nangurugwai - Mbwemkuru - Miluwi - Kiangara kama njia mbadala ili kusaidia kuifungua Wilaya ya Liwale kutokana na barabara hiyo kuathirika kidogo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa wanaendelea kusimamia maelekezo ya viongozi wa kitaifa ili kuhakikisha maeneo yote yenye changamoto yanapatiwa ufumbuzi na kuweza kufikika kama ilivyo kuwa awali.
Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama amesema Serikali imejipanga kuwasaidia wananchi wote ambao maeneo yao hayapitiki na wanakosa huduma muhimu za kijamii “Tumeweka mpango wa kuwasaidia kuhakikisha wanapata chakula kitakachowasaidia hadi pale miundombinu itakapokuwa imeimarika, tutaanza kutoa magari mengine ya chakula Dar es Salaam”