Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Amkaribisha Dkt. Biteko Ofisini
Sep 02, 2023
Waziri Mkuu Amkaribisha Dkt. Biteko Ofisini
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakati aliporipoti ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri Mkuu, Kassim, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhandisi Cyprian Luhemeja, kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, Septemba 2, 2023.
Na Ofisi wa Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa leo Septemba 2, 2023, amemkaribisha Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Doto Biteko katika ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyopo Magogoni jijini Dar es Salaam na amemuahidi kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiongezea nguvu Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kumteua Mhe. Dkt. Biteko kuwa Naibu Waziri Mkuu ili waweze kusimamia uratibu shughuli za Serikali kwa pamoja.

"Kwa niaba yenu, Mhe. Naibu Waziri Mkuu tunakukaribisha sana hapa katika ofisi yetu na tunakupongeza kwa kuaminiwa na Mhe. Rais kupewa jukumu kubwa la Naibu Waziri Mkuu kwa lengo la kusimamia shughuli za Serikali. Nakuhakikishia kwamba una timu imara ambayo inatoa ushirikiano wakati wote.” Alisema Mhe. Majaliwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo na ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano. Amewaomba watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wafanye kazi kwa bidii ili maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia na Watanzania yaweze kufikiwa.

Viongozi wengine walioshiriki mapokezi hayo ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako.

Wengine ni Naibu Waziri Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri wa Nchi ( Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhandisi Syprian Luhemeja na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi