Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Akutana na Makampuni ya Madini Kutoka Korea
Sep 03, 2023
Waziri Mkuu Akutana na Makampuni ya Madini Kutoka Korea
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mjumbe Maalum wa Rais wa Korea Kusini, Bw. Yoon Sang Jick wakati alipokutana na ujumbe kutoka Korea Kusini uliyoambatana na Makampuni makubwa ya madini, kwenye Ukumbi wa BOT jijini Dar es salaam, Septemba 2, 2023.
Na Ofisi wa Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amekutana na ujumbe kutoka Korea Kusini uliojumuisha viongozi wa makampuni makubwa ya madini yanayohusika na mnyororo wa thamani wa uzalishaji betri za magari ya Posco Holdings, Posco International,SK, Korea Zinc na LX International.

Mhe. Majaliwa amewahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali ya Tanzania ipo tayari kwa uwekezaji wao na itawawezesha kuwekeza mitaji yao.

“Sisi tuna madini na ninyi ndugu zetu Wakorea mna mitaji, twende tuunganishe nguvu kwa manufaa ya nchi zetu.” alisema Waziri Mkuu.

Ameyasema hayo jana (Jumamosi, Septemba 2, 2023) alipokutana na ujumbe wa Korea Kusini na kujadili kuhusu ushirikiano katika uendelezaji wa madini ya kimkakati nchini Tanzania.

“Ninapenda kuwahakikishia kuwa nchi yetu ni salama na Mhe. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kila linalowezekana kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.”

Waziri Mkuu amesema Serikali imeimarisha mazingira ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya usafirishaji kama barabara, ndege na nishati ya kutosha kwa ajili ya uendeshaji wa viwanda. “Lengo ni kuhakikisha kila muwekezaji anayekuja anapata faida kutokana na uwekezaji wake.”

Kwa upande wake, Mjumbe Maalumu wa Rais wa Korea ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe huo kutoka Korea Kusini, Bw. Yoon Sang Jick ameishukuru Serikali ya Tanzania na kwamba wataendelea kushirikiana nayo kuhakikisha malengo ya uwekezaji yanafanikiwa.

Naye, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameishukuru Korea Kusini kwa kuichagua Tanzania na kufanya mazungumzo kuhusu uwekezaji katika sekta ya madini. Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo kuja kuwekeze Tanzania.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi