Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mhagama Akabidhi Magari na Pikipiki vya Zaidi ya Bilioni Mbili kwa Watekelezaji wa AFDP
Mar 12, 2024
Waziri Mhagama Akabidhi Magari na Pikipiki vya Zaidi ya Bilioni Mbili kwa Watekelezaji wa AFDP
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi vitendea kazi (Magari na pikipiki) kwa watekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) tarehe 12 Machi, 2024 katika halfa ya kukabidhi vifaa hivyo iliyofanyika katika viwanja vya ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu – Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama amekabidhi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa watekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP)  Mapema leo tarehe 12 Machi, 2024 katika viwanja vya ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma.


Akikabidhi vifaa hivyo ambavyo ni magari, pikipiki za miguu miwili na mitatu (guta) kwa wawakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi,  Wizara ya Kilimo, Wakala wa Mbegu (ASA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Taasisi za Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI) na Mratibu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Waziri Mhagama alieleza kuwa upatikanaji wa vifaa vinavyonunuliwa kupitia Programu hiyo ikiwemo magari na pikipiki, ni vitendea kazi muhimu katika utekelezaji wa Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 bila ya kusahau  ununuzi wa meli nane (8) kwa ajili ya uvuvi katika bahari kuu na kuendeleza ukuzaji viumbe maji, na kilimo cha  Mwani.


“Vilevile, Programu hii inalenga kuongeza uzalishaji, tija na faida katika shughuli za wakulima kwa kuendeleza shughuli za ugunduzi na uzalishaji wa mbegu bora na kuhamasisha kilimo cha mazao lishe (nutritional sensitive) ili kupunguza udumavu.” Alifafanua Waziri Mhagama


Aliendelea kusema kuwa programu hiyo inaenda kuleta mabadiliko makubwa kwenye uzalishaji na uendelezaji wa biashara kwa kuzingatia mazingira halisi yaliyopo na hasa uboreshaji wa uzalishaji wa mbegu za mazao ya kilimo, mahindi, alizeti, maharage na mimea jamii ya kunde pamoja na uboreshaji wa sekta ya uvuvi, mifugo na ufugaji wa viumbe maji kwa lengo la kuwaendeleza na kuwawezesha akina mama na vijana wa kitanzania kunufaika zaidi na sekta hizo mbili.
 



Akizungumza kwa Niaba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar), Mheshimiwa Hamza Hassan Juma alisema matunda ya mafanikio haya ni matokeo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Shekhe Abeid Amani Karume takribani miaka sitini iliyopita, “kwenye zoezi hili kuna kipengele cha ununuzi wa meli za uvuvi ambazo tutazipata sisi kutokana na faida ya Muungano wetu.” Alibainisha



Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde alisema vifaa hivyo vitaenda kuchochea kasi ya utekelezaji katika sekta ya kilimo hasa katika shughuli mbalimbali zilizopangwa katika utekelezaji wa program hiyo na kutoa rai kwa taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo zinahakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa  malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kufikia malengo ya Programu.

 

 Baadhi ya vifaa vilivyokabidhiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama kwa watekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP)  Mapema leo tarehe 12 Machi, 2024 katika halfa ya kukabidhi vifaa hivyo iliyofanyika katika viwanja vya ofisi hizo zilizopo Mtumba jijini Dodoma.
 



Akiongea kwa Niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Riziki Shemdoe alisema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongonzwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kuendeleza sekta ya uvuvi nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi ya bandari ya uvuvi Kilwa Masoko ambapo Meli za uvuvi za kibiashara zitakazonunuliwa kutokana na program ya (AFDP) zitatia nanga katika bandari hiyo.



Awali akiongea katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bw. Anderson Mutatembwa alisema lengo kubwa la Progrmamu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) kuchangia katika mfumo jumuishi ya chakula ili kuboresha maisha, usalama wa chakula, lishe na ustahimilivu kwa kuongeza uzalishaji pia kuongeza ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na biashara ya baadhi ya mazao ya uvuvi na ufugaji wa viumbemaji na jumla ya kaya 260,000 zinatarajiwa kufikiwa katika program hii katika mikoa 11.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi