Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mabula Aonya Changamoto Ukosefu wa Uadilifu Sekta ya Uthamini Nchini
Oct 20, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula ameonya Wataalamu wa Taaluma ya Uthamini nchini kuacha na tabia zinazo dhalilisha taaluma ikiwemo ukosefu wa uadilifu katika suala zima la kuongeza ukadiliaji thamani usiozingatia uhalisia.

Dkt. Mabula amesema kuna baadhi ya Wathamini kwa kushirikiana nawahusika wakiwemo walipa fidia, wananchi wenye mali, maafisa wa taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwauthamini wa mali za rehani, kuongeza au kupunguza thamani tofauti na uhalisia ili kutoa unafuu kwa upande husika jambo ambalo amesema lina athari kwa mapato ya Serikali na kuitaka Bodi ya Wathamini kuwachukulia hatua pindi watakapobainika.

Aidha, Dkt. Mabula ameangazia pia suala la kuandikia na kujumuisha kwenye taarifa za fidia mali “hewa” yaani mali ambazo hazipo uwandani na wakati mwingine kuondoa na kutojumuisha kwenye taarifa ya fidia baadhi ya mali zilizopo uwandani katika taarifa ili kukidhi matakwa ya mteja wake anayetaka, hata kwa kutumia rushwa, unafuu wa fidia katika eneo husika.

Dkt. Mabula ameyasema hayo leo Oktoba 20, 2022 wakati akitoa hotuba ya ufunguzi kwa Wathamini mali katika Mkutano Mkuu wa tatu wa Wathamini unaoendelea kwa siku mbili jijini, Arusha.

“Vitendo vya aina hii vinaichafua taaluma hii, hivyo, naitaka Bodi kuchukua hatua kali zaidi kwa Wathamini watakaobainika na Makampuni yatakayojihusisha na vitendo vya aina hii, kwenye swala hili, naomba Bodi yako iwachukulie hatua wathamini wote bila kujali kama ni wa Serikali au wa kutoka sekta binafsi, kwa kuwa wote ni taaluma moja na sheria haingalii sekta binafsi wala mwajiriwa Serikalini”, aliongeza Dkt. Angeline Mabula.  

Dkt. Mabula amemtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Wathamini kutoa taarifa kwa Serikali ikiwa Mthamini mhusika ni wa Serikali ili Wizara iangalie namna ya kuchukua hatua stahiki kwa mtumishi kulingana na sheria za ajira ya Serikali.

Waziri Mabula ameiagiza Bodi ya taaluma hiyo kuwa, yale watakayoweza kuyafanyia kazi kupitia Mkutano huo wayatekeleze kwa maarifa yao na juhudi zao zote na yale ambayo yatahitaji muda waweke mikakati mipya ya kuyatekeleza.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi amewataka Wathamini hao kuangalia namna bora ya kutoa maoni ili Wizara yake iweze kufanya maboresho katika sheria ya wathamini na Serikali iweze kukuza uchumi kutokana na taaluma hiyo.

Aidha, Dkt. Kijazi amewataka wataalamu hao kuangalia kutoa mrejesho wa namna bora ya kuboresha mahusiano kiutendaji kazi kutokana na kuwepo mkanganyiko wa kimtazamo na kiutendaji unaotokana na tofauti zao katika ajira hususani kati ya waajiriwa serikalini na sekta binafsi.

“Tungependa kama Wizara kuona mkiboresha uhusiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi na kwamba mna mawasiliano ya mara kwa mara binafsi pia naelewa kumekuwepo na mitizamo binafsi nyingine chanya na nyingine hasi, hivyo kuboresha uhusiano katika utendaji kazi kutasaidia kuwahudumia Watanzania vizuri Zaidi kuliko ilivyo wakati huu”, alisema Dkt. Kijazi.

Mkutano wa tatu wa Mwaka wa taaluma ya Wathamini pamoja na mambo mengine, umepokea wanataaluma wapya 53 ambao wamesajiliwa na Bodi ya Taaluma ya Wathamini baada ya kuwa wameshinda mitihani ya bodi hiyo na kusajiliwa na bodi hiyo.      

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi