Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Jafo Ashiriki Mkutano wa UNEA6 Kenya
Feb 27, 2024
Waziri Jafo Ashiriki Mkutano wa UNEA6 Kenya
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akishiriki Mkutano wa Sita wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA6) unaofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) jijini Nairobi, Kenya ambapo ulifunguliwa Februari 26, 2024 na kutarajiwa kuhitimishwa Machi 01, 2024.
Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo anashiriki Mkutano wa Sita wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA6) unaofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) jijini Nairobi, Kenya.

 

Kupitia mkutano huo, viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania wanajadili namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa baionuai na uchafuzi wa mazingira.

 

Kama inavyofahamika Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha ukame, uhaba wa mvua, mafuriko na vifo vya mifugo.

 

Pamoja na kushiriki Mkutano wa UNEA6, katika kukabiliana na changamoto hizo Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha taifa linakuwa salama.

 

Lengo la mkutano huo ni kuunda sera kuhusu mazingira ambapo UNEA linalenga kurejesha maelewano kati ya binadamu na mazingira na hivyo kuboresha maisha ya watu wanaokabiliwa na changamoto za mazingira.

Hivyo, mkutano huo ni fursa pia kwa serikali za nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, wanaharakati wa mazingira, wanasayansi na sekta binafsi kupaza sauti na kuhusishwa katika kutunga sera ya ulimwengu mzima kuhusu mazingira.

Ujumbe wa Tanzania umeambatana na Waziri Dkt. Jafo na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi na wataalamu kutoka Ofisi hiyo. 

Mkutano huo wenye kaulimbiu ‘Juhudi madhubuti, jumuishi na endelevu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa bayoanuai na uchafuzi‘ unatarajiwa kuhitimishwa Machi 01, 2024.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi