Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Jafo Aiomba FAO Kuunga Mkono Serikali Usimamizi wa Mazingira
Mar 04, 2024
Waziri Jafo Aiomba FAO Kuunga Mkono Serikali Usimamizi wa Mazingira
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Bi. Maria Helena Semedo (hayupo pichani) katika Mkutano wa Uwili wakati wa Mkutano wa Sita wa Baraza wa Mazingira Duniani (UNEA6) jijini Nairobi nchini Kenya. Kulia ni Afisa Mazingira Mwandamizi Ofisi ya Makamu wa Rais, Simeon Shimbe.
Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameliomba Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kuendelea kuunga mkono mipango ya Serikali ya Tanzania katika usimamizi wa mazingira na kupambana na athari za mabadilko ya Tabianchi. 

 

Pia, ameolimba shirika hilo kuisaidia Tanzania kiteknolojia, ubunifu, mafunzo na masuala ya kifedha kwa miradi ya maendeleo katika Sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi hususan Ajenda 10/30.

 

Ametoa ombi hilo alipokutana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Bi. Maria Helena Semedo katika Mkutano wa Uwili jijini Nairobi nchini Kenya wakati wa Mkutano wa Sita wa Baraza wa Mazingira Duniani (UNEA6).

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza jambo na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Bi. Maria Helena Semedo mara baada ya kufanyika Mkutano wa Uwili wakati wa Mkutano wa Sita wa Baraza wa Mazingira Duniani (UNEA6) jijini Nairobi nchini Kenya.

Katika kikao hicho kilicholenga kuimarisha uhusiano baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na FAO, Dkt. Jafo amelishukuru kwa kazi kubwa wanayofanya nchini tangu Tanzania ijiunge na shirikia hilo mwaka 1962 na tangu shirika hilo lilipofungua ofisi zake nchini mwaka 1977. 

 

Ameongeza kuwa FAO imekuwa ikishirikiana vyema na Tanzania katika kujengea uwezo wataalamu wa Serikali, kusaidia katika usalama wa chakula sambamba na sekta ya kilimo, mazingira na masuala mbalimbali ya kimaendeleo. 

 

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu, Bi. Semedo amemuhakikisha Waziri Dkt. Jafo na Serikali ya Tanzania kwamba FAO itaendelea kudumisha ushirikiano wao kwa kuweka nguvu katika sekta ya mazingira.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Bi. Maria Helena Semedo (katikati) mara baada ya Mkutano wa Uwili wakati wa Mkutano wa Sita wa Baraza wa Mazingira Duniani (UNEA6) jijini Nairobi nchini Kenya.

Halikadhalika, ameihakikishia Tanzania kuwa shirika litaendeleza utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo hususan kuongeza tija katika kilimo ili Tanzania iweze kufikia malengo iliyojiwekea.

 

Itakumbukwa kuwa Mkutano UNEA6 huo uliofanyika Februari 26 hadi Machi Mosi, 2024 ulichagizwa na kaulimbiu 'Juhudi Madhubuti, Jumuishi na Endelevu za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, Uharibifu wa Bioanuai na Uchafuzi‘. 

 

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri Dkt. Jafo akiambatana na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi pamoja na wataalamu kutoka ofisi hiyo. 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi